Ghani na Abdullah wasaini makubaliano
21 Septemba 2014Wapinzani wawili wa kisiasa waliokuwa wakigombea wadhifa wa Urais nchini Afghanistan wametia saini makubaliano ya kugawana madaraka baada ya miezi kadhaa ya mvutano uliosababishwa na matokeo ya uchaguzi yaliyoleta utata na kuzusha hali ya ukosefu wa usalama katika wakati ambapo nchi hiyo inajiandaa kubakia peke yake bila ya vikosi vya usalama vya kigeni.
Ashraf Ghani aliyekuwa waziri wa fedha ambaye anachukuwa wadhifa wa urais kwa mujibu wa makubaliano hayo yaliyofikiwa Jumamosi usiku ameridhia kushirikiana na Abdullah Abdullah baada ya kusaini makubaliano hayo katika sherehe iliyoonyeshwa moja kwa moja kupitia Televisheni. Serikali mpya inakabiliwa na changamoto kubwa katika kupambana na uasi unaoongozwa na wapiganaji wa Taliban pamoja na suala la kulipa madeni yake kufuatia kuporomoka kwa mapato ya kodi.
Halikadhalika itakabiliwa na matatizo makubwa katika kuhakikisha inaimarisha maisha ya raia wa kawaida wa taifa hilo wanaokabiliwa na wakati mgumu kutokana na kupungua kwa kasi ya misaada na pia kutokana na vikosi vya Jumuiya ya Nato kujiandaa kuondoka nchini humo kufikia mwishoni mwa mwaka huu.
Makubaliano ya kugawana madaraka yalitiwa saini ingawa matokeo ya mwisho ya duru ya pili ya uchaguzi wa Juni 14 uliozusha ubishi mkubwa,hayajatangazwa.Na kwa mujibu wa msemaji wa rais anayeondoka madarakani,Hamid Karzai,Aimal Faizi,Ghani anatarajiwa kuapishwa madarakani kama rais wa taifa hilo ndani ya kipindi cha wiki moja.
Kikubwa ambacho anatarajiwa kukipa kipaumbele pindi akitwaa madaraka ni kuyatia saini makuabaliano ya kiusalama yaliyocheleweshwa kwa muda mrefu kati ya taifa hilo la Marekan,ambayo yataruhusu kubakishwa wanajeshi wachache wakigeni baada ya mwaka 2014.Marekani imepongeza hatua ya kufikiwa makubaliano ya kugawana madaraka ambayo yalisimamiwa na waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo John Kerry.
Ikulu ya Marekani imetowa taarifa ikisema makubaliano hayo ni mwanzo wa nafasi muhimu ya mshikamano pamoja na usalama thabiti wa taifa hiloAidha Marekani imewatolea mwito waafghanistan wote ikiwemo viongozi wa kisiasa,kidini na kiraia kuunga mkono makubaliano hayo na kushirikiana pamoja kutoa mwito wa ushirikiano na utulivu.
Ikumbukwe kwamba kambi za wanasiasa hao wawili Ghani na Abdullah zilikutana jumamosi usiku kujaribu kumalizia makubaliano hayo kabla ya kutolewa matokeo ya uchaguzi yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa.Tume huru ya Uchaguzi imefahamisha kwamba itatangaza matokeo rasmi ya mwisho baadae leo Jumapili,ingawa hakuna muda mmalum uliotolewa wa hatua hiyo kufanyika.
Chini ya makubaliano ya kugawana madaraka,Asraf Ghani atakuwa rais mpya wa Afghanistan wakati Abdullah Abdullah atachukuwa jukumu la kumteua atakayekuwa afisa mtendaji mkuu,ambao ni wadhifa mpya nchini humo na ambao ni sawa na nafasi ya waziri mkuu,jambo ambalo linaweza kusababisha mauzauza katika wizani wa madaraka wakati nchi hiyo ikiingia katika enzi mpya.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri:Sudi Mnette