Ghani aapishwa kuwa rais mpya Afghanistan
29 Septemba 2014Hiyo ni mara ya kwanza kwa nchi hiyo kukabidhi madaraka kwa njia ya kidemokrasia tangu operesheni ya mwaka wa 2001 iliyoongozwa na Marekani kuuangusha utawala wa Taliban.
Muda mfupi baada ya Ghani Ahmadzai kula kiapo, alimwapisha aliyekuwa mpinzani wake katika uchaguzi uliopita, Abdullah Abdullah, kama mtendaji mkuu, na kutimiza ahadi ya kisiasa aliyotoa ya kugawana madaraka na kuondoa malumbano ya kisiasa ambayo yalitishia kuzusha machafuko baina ya pande za kaskazini na kusini mwa nchi hiyo.
Katika hotuba yake ya kwanza, rais Ghani ametoa wito kwa wapiganaji wa Taliban na wanamgambo wengine kuungana katika mchakato wa kisiasa nchini humo na kuweka chini silaha. Hata hivyo, machafuko yaliyosababishwa leo na wanamgambo wenye itikadi yamewauwa karibu raia 12 wakiwemo polisi, wakati majeshi ya kigeni yakijiandaa kuondoka nchini humo ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
Akizungumza moja kwa moja kupitia televisheni, Ghani, ambaye ni afisa wa zamani wa Benki ya Dunia na waziri wa fedha wa Afghanistan alisema nchi imechoshwa na vita. Abdullah, ambaye ni waziri wa zamani wa mambo ya nchini za kigeni, alimpongeza kwanza rais anayeondoka Hamid Karzai kwa uongozi wake pamoja na watu wa Afghanistan kwa kujitokeza kwa wingi na kupiga kura zao licha ya kitisho cha mashambulzii kutoka kwa wanamgambo wa Taliban ambao walijaribu kuvuruga mchakato wa uchaguzi. Ghani kisha alimpongeza Karzai kwa kukabidhi madaraka kwa njia ya amani na ya kidemokrasia, na pia akamshukuru Abdullah kwa kuufanikisha mpango wa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa. Karzai aliwapongeza viongozi hao wapya
Miongoni mwa waliohudhuria sherehe hiyo ni John Podesta, mshauri wa rais wa Marekani Barack Obama, Rais wa Pakistan Mamnoon Hussain na Makamu wa Rais wa India Mohammad Hamid Ansari. Maafisa wa Marekani wanasema wanataraji rais Ghani kusaini muafaka wa wa usalama baina ya Afghanistan na Marekani ili kuwaruhusu karibu wanajeshi 10,000 wa Marekani kusalia nchini humo baada ya kukamilika operesheni ya kimataifa ya kupambana na Taliban mnamo Desemba 31 mwaka huu.
Lakini kwa waafghanistani waliokuwa wakifuatilia shughuli hiyo ya kuapishwa serikali mpya, kitisho cha machafuko na ukosefu wa usalama vinasalia kuwa mojawapo ya mambo yanayowakosesha usingizi.
Mwandishi: Bruce Amani/AP
Mhariri: Iddi Ssessanga