1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghana yawageuka wenziwe mzozo wa Cote d'Iviore

Admin.WagnerD7 Januari 2011

Mzozo wa kisiasa nchini Cote d'Ivoire umechukua mwelekeo mpya baada ya serikali ya nchi jirani ya Ghana kujitenga nao, huku ikisisitiza kuwa matumizi ya nguvu za kijeshi si suluhu.

https://p.dw.com/p/zuse
Machafuko baada ya uchaguzi wa Novemba 2010 nchini Cote d'ivoire
Machafuko baada ya uchaguzi wa Novemba 2010 nchini Cote d'ivoirePicha: AP

Akizungumza na waandishi wa habari, Rais wa Ghana, John Atta Mills, alisema nchi yake kamwe haitomuunga mkono yeyote katika mvutano huo wa kisiasa ambao umeendelea kwa muda wa zaidi ya mwezi mmoja.

Hata hivyo, Rais Mills amesisitiza kuwa ataiunga mkono serikali itakayofanikiwa kuingia madarakani na ana imani kuwa diplomasia ndiyo suluhu ya pekee iliyosalia.

Kwa upande wake, Jumuiya ya Uchumi ya Afrika ya Magharibi, ECOWAS, bado inashikilia msimamo wake wa kumtaka Gbagbo kuachia madaraka, vyenginevyo akabiliane na nguvu za kijeshi.

Licha ya kuwa Ghana ni mwanachama wa jumuiya hiyo na Rais Mills kuonesha kukubaliana na uamuzi wao wa kumtaka Gbabo awachie madaraka, lakini haiungi mkono matumizi ya nguvu za kijeshi.

Ili kulitilia mkazo suala hilo,Waziri wa Ulinzi wa Ghana amesema kuwa nchi yake kamwe haitopeleka wanajeshi kama sehemu ya kikosi kitakachomuondoa Gbago kwa nguvu.

Viongozi wa Jumuiya ya Uchumi ya Afrika ya Magharibi, ECOWAS, wakikutana na Lautent Gbagbo mjini Abdijan, kumrai aondoke madarakani kwa hiari
Viongozi wa Jumuiya ya Uchumi ya Afrika ya Magharibi, ECOWAS, wakikutana na Lautent Gbagbo mjini Abdijan, kumrai aondoke madarakani kwa hiariPicha: AP

Kulingana na Waziri huyo, matumizi ya nguvu hizo huenda yakasababisha ghasia na machafuko, jambo litakalowafanya raia wengi wa Cote d'Ivoire kutafuta hifadhi nchini Ghana. Ifahamike kuwa kiasi ya wanajeshi 500 wa Ghana wanashiriki katika kikosi cha walinda amani wa Umoja wa Mataifa kilichopo Cote d'Ivoire, MINUCI.

Wiki iliyopita, maafisa wa kulinda usalama wafuasi wa Alassane Ouattara waliwakamata raia watano wa Ghana wanaoshukiwa kuwa mamluki walioagizwa na Gbagbo. Uongozi wa Ghana umeyakanusha madai hayo.

Wakati huo huo, mataifa ya Magharibi yanazidi kuimarisha harakati zake za kumtenga Gbagbo kwa kumuwekea vikwazo maalum. Marekani tayari imeshamuwekea Gbagbo na wapambe wake vikwazo vya usafiri na kuwapiga marufuku raia wake kufanya biashara na kundi hilo.

Umoja wa Ulaya, kwa upande wake, umetahadharisha kuwa unajiandaa kuufuata mkondo huo kwa kuzibana fedha za Gbagbo ndani ya kipindi cha wiki chache zijazo.

Kwa upande mwengine, mahakama moja nchini Cote d'Ivoire imewaachia huru maafisa 22 wa ngazi za juu wa sekta ya kakao, waliokuwa wakizuiliwa kwa sababu ya mashtaka ya ubadhirifu yaliyokuwa yakiwakabili tangu mwaka 2008. Viongozi hao wameachiwa huru wakisubiria hukumu kamili ya mahakama.

Kesi hiyo iliacha kusikilizwa tangu wakati wa pirikapirika za uchaguzi wa rais na duru ya pili iliyofanyika mwishoni mwa mwezi wa Novemba mwaka jana. Wengi ya maafisa hao walioachiwa ni washirika wa karibu wa Gbagbo.

Cote d'Ivoire inaongoza kwa kuzalisha zao la kakao duniani na zao hilo huchangia kiasi cha asilimia 40 ya fedha zake za kigeni.

Mwandishi: Mwadzaya,Thelma/RTRE/AFPE

Mhariri: Josephat Charo