Ghana yatoka sare na Australia bao 1:1
19 Juni 2010Ghana na Australia, zime chapana bao 1:1 huko Rustenburg, na Ghana imeshika usukani wa kundi hili D ,mbele ya Ujerumani na Serbia. Baada ya Australia , kutangulia kwa bao la kwanza tayari mnamo dakika ya 11 ya mchezo kufuatia mkwaju wa freekick ambao kipa wa Ghana,Kingston, alishindwa kuudhibiti mpira,Ghana haikukawia klujibisha. Mensa, aliuchapa mkwaju mkali katika lango la Australia baada Ayew, mtoto wa Abedi Pele, kuwachenga walinzi wa Australia, maridadi ajab na kuutia kati ya eneo la adhabu la Australia.
Mlinzi wa Australia,akauzuwia mpira kwa mkono katika lango lake na hii ikaongoza bao la penalty kwa Ghana alilotia Assamoah . Ni yeye alietia pia bao la penalty Ghana ilipocheza na Serbia.Mlinzi wa Australia akapigwa kadi nyekundu na kuwaacha Waaustralia kama wajerumani jana wanacheza na watu 10. Sasa Ghana inasubiri mpambano na Ujerumani kujua hatima yake iwapo kama Kombe la Dunia 2006 nchini Ujerumani,itacheza duru ya pili au la.Ghana,ilikua na nafasi ya kuamua hatima yake leo ,lakini ilifanya uzembe .
Kabla ya Ghana na Australia, kuteremka uwanjani ,Holland iliizaba Japan bao 1:0 na kuongezea pointi 3 nyengine katika zile ilizonyakua kutoka Denmark kwa kuilaza mabao 2:0 katika mpambano wao wa kwanza.
Bao la Weslie Sneider, mnamo dakika ya 52 ya mchezo lilitosha kuvunja tumbuu ya lango la wajapani ambao binafsi, pia hasa dakika za mwisho za mchezo, walikua hatari sana katika lango la Holland. Orgasaki, alikosea mara 2 kusawazisha na hasa mnamo dakika ya 90 ya mchezo. Ghana ikijitahidi kuondoka na ushindi mwengine na Australia ikijilinda,
Dola nyingi za kabumbu zilizopigiwa upatu zingetawazwa mabingwa wa dunia 2010 huko Afrika Kusini, hapo Julai 11, zimeteleza:Baada ya Spain ,Ufaransa na hata mabingwa watetezi-Itali, jana ilikua zamu ya Waingereza na Wajerumani, kufunzwa darasa la dimba:kuwa mpira unadunda.
Uingereza, ilizimwa na Waalgeria,waliocheza kwa kasi na kuwazima akina Wayne Rooney,Heski na Steven Gerrda-nahodha wao na sasa jahazi la kocha Fabio Capello,linaenda mrama na mashabiki wao wawazomea Waingereza wakihanikiza zaidi hata kupita vuvuzela.
Ujerumani, nayo ilikiona kilichomtoa kanga manyoya mbele ya Serbia ilipokomewa bao 1:0.
Baada ya Ujerumani, kuizaba Australia mabao 4:0 katika mpambano wao wa kwanza ,Ujerumani, ilipanga kufuata mkondo ule ule mbele ya Waserbia,lakini mnamo dakika ya 37 ya mchezo ,mshambulizi Miroslav Klose,alitolewa na rifu nje ya uwanja kwa kucheza ngware.Stadi wa Serbia, Milan Jovanovic, akaitumia nafasi hiyo na kuipatia Serbia bao. Kipa wa Serbia,Vladmir Stojkovic, akawa shujaa wa Waserbia alipozuwia mkwaju wa penalti wa Lukas Podolski, na kuinyima Ujerumani mnamo dakika ya 60 ya mchezo nafasi ya kusawazisha kufanya matokeo 1:1:
Baadae,Lukas Podolski, alievurumisha mikwaju mingi katika lango la Serbia bila mafanikio aliuelezea mchezo huo ,
"Nadhani, tulicheza uzuri na hata kipindi cha pili tulipobidi kucheza na wachezaji 10 tu.Kadi nyekundu ambayo rifu alivuka mpaka kuitoa, ilituharibia mchezo na halafu mkwaju wangu wa penalti uliozuwiliwa na kipa .Hizo ni sababu 2: kwanini tulishindwa na Serbia.Sasa, baada ya siku chache, itatupasa kuishinda Ghana." Ujerumani, imeiona Ghana ikitikiswa hadi dakika ya mwisho na Australia na itaishinikiza mno kupata ushindi inaohitajia kwa kila hali.Ujerumani ina miadi na Ghana, Jumatano ijayo, wakati hatima ya Uingereza ,itaamuliwa na Slovenia iliotoka sare jana 2:2 na Marekani.
Mwandishi: Ramadhan Ali /DPAE
Uhariri: Mohamed Dahman