Ghana yasubiri matokeo ya uchaguzi
9 Desemba 2016Ghana ingali bado imegubikwa na wasiwasi, wakati raia wake wakisubiri kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais yanayotarajiwa kuanza kutolewa na tume ya uchaguzi leo hii, ingawa tayari wafuasi wa upinzani walianza kushangiria ushindi tangu jana, na ijumaa hii rais aliyeko madarakani John Mahama anayepigania muhula wa pili akisema kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba ataifanya Ghana kuendelea kujivunia, bila kujali matokeo hayo yatakuwaje.
Taarifa zilizotolewa ijumaa hii kupitia vituo viwili binafsi vya redio nchini humo zimesema mgombea kupitia upinzani Nana Akufo-Addo ameshinda, baada ya kumpita kwa kura nyingi mpinzani wake Rais Mahama. Vituo hivyo vya Joy FM na Citi FM, ambavyo ni miongoni mwa vituo vinavyoheshimika zaidi nchini Ghana, vimetangaza ushindi huo kwa kuzingatia sura ya matokeo ya majimbo, katika uchaguzi huo uliofanyika Jumatano hii.
Kwenye ukurasa wake wa Twitter, Rais Mahama pamoja na kueleza kuifanya Ghana kuendelea kujivunia, ametaka kupewa muda kwa tume ya uchaguzi ili iendelee kutekeleza majukumu yake ya kikatiba.
Kulingana na matokeo yaliyotangzwa na kituo cha Joy FM, Akufo-Addo ameshinda kwa asilimia 53, huku Mahama akipata asilimia 45.15. Vituo hivyo vimezingatia kura ambazo tayari zimehesabiwa katika majimbo 217 kati ya 275. Kituo cha Citi FM kimempa Akufo-Addo ushindi wa asilimia 54.8 kwa kuangazia kura zilizohesabiwa kwenye majimbo 190.
Awali, Akufo-Addo aliwahutubia wafuasi wa chama chake cha New Patriotic, NPP, na kuwaambia alikuwa na uhakika wa kumshinda Mahama pamoja na kwamba tume ya uchaguzi bado haijatangaza matokeo rasmi.
Mmoja wa wafuasi wa chama hicho cha NPP, Osei Kwaku Anyemedu, alipozungumza na mwandishi wa DW Katrin Gansler amesema ana furaha sana kwa chama hicho kuibuka na ushindi, kwa kuwa wanahitaji kuona mabadiliko.
Mwenyekiti wa tume hiyo, Charlotte Osei, alisema kwenye mkutano na waandishi wa habari kitu cha msingi zaidi ni uhakika wa matokeo hayo kuliko haraka, na kuwataka raia kuwa wavumilivu.
Matokeo yaliyotolewa na timu ya ya Akufo-Addo yameongeza wasiwasi kwa tume ya uchaguzi, kutokana na madai kwamba matokeo ya ndani kutoka vituo mbalimbali yanaonyesha mpinzani huyo alikuwa akiongoza kwa zaidi ya kura milioni moja. Msemaji wa NPP, Oboshie Sai Cofie, alisema ilikuwa dhahiri kwamba chama hicho kimeshinda.
Hata hivyo, Naibu Katibu mkuu wa chama tawala cha NDC, Koku Anyidohu, amepingana na taarifa hizo na kuziita kuwa ni proraganda. Amesema kutoa matokeo ya ndani ni kinyume ca sheria na kunalenga kuvipotosha vyombo vya habari. Waangalizi nao wameendelea kuishinikiza tume hiyo kuharakisha mchakato wa kutangaza matokeo.
Mwandishi: Lilian Mtono/AFPE/RTRE
Mhariri: Mohammed Khelef