1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghana yafunga maduka ya wageni

6 Julai 2012

Serikali ya Ghana haitaki mchezo. Tokea wiki hii biashara na vibanda vya raia wa nje vinafungwa. Vikosi maalumu vinaifanya kazi hiyo. Milango ya maduka na ya vibanda inatiwa kufuli.

https://p.dw.com/p/15T1Y
Wauzaji Ghana
Wauzaji GhanaPicha: picture-alliance/dpa

Serikali ya Ghana imepitisha sheria inayowaathiri wafanyabiashara kutoka nchi za nje ikiwa pamoja na Waafrika wanaotoka nchi zilizomo katika jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS. Sheria hiyo inawataka wafanyabiashara hao wafungue biashara zao kwenye sehemu zilizotengwa maalumu, kila mfanyabiashara wa nje afungue biashara yenye thamani ya dola 300,000 na lazima awaajiri wananchi wa Ghana angalau kumi.


Waziri wa biashara wa Ghana Hannah Tetteh amesema kuwa lengo la sheria hiyo ni kuyalinda maslahi ya wafanyabiashara wazalendo na amekanusha madai kwamba sheria hiyo inawanyima haki raia wa nchi nyingine na kuharibu mazingira mazuri ya kufanyia biashara Ghana. Naye waziri wa mabo ya kigeni wa nchi hiyo, Alhaji Muhammed Mumuni, amepinga shutumua kwamba sheria mpya ya biashara inakiuka mikataba ya ECOWAS inayotaka raia wote wa nchi mwanachama wapewe haki ya kuingia na kuishi katika nchi yoyote ya jumuiya hiyo bila kizuizi.

Wageni wengi wanaendesha biashara ndogo ndogo
Wageni wengi wanaendesha biashara ndogo ndogoPicha: DW

Wanigeria wengi wanafanya biashara ndogo ndogo tu

Lakini sheria hiyo imeshasababisha mvutano baina ya Ghana na nchi nyingine za Afrika magharibi kama Nigeria. Wabunge wa nchi hiyo sasa wanataka Nigeria ivunje uhusiano wa kibalozi na Ghana. "Wafanyabiashara wengi kutoka Nigeria wanafanya biashara ndogo kama vile kuuza CD, mikanda ya video pamoja kaseti za redio. Watawezaje kupata mtaji wa dola 300,000 unaohitajika kuanzisha biashara?" aliuliza mbunge mmoja, Abike Dabiri-Erewa.

Hofu imetanda miongioni mwa wafanyabiashara wa kigeni waishio Ghana. Amaefola Chijoke, raia wa Nigeria, anauza simu za mkononi katika barabara ya Kwame Nkrumah iliopo Accra, mji mkuu wa Ghana. Yeye anaeleza kwamba wafanyabiashara kama yeye hawajahamia Ghana wakiwa na lengo la kuyaathiri maisha ya Waghana bali wanakimbia umasikini nchini mwao. Mfanyabiashara mwingine wa Kihindi amelalamika kwamba tayari ameshawekeza mamilioni katika uchumi wa Ghana lakini anahofia kwamba hilo halizingatiwi tena. "Kwa kweli hatuji tufanye nini," alieleza mfanyabiashara huyo.

Mwandishi: Elizabeth Shoo
Mhariri: Mohammed Khelef