1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghana yafanya uchaguzi mkuu

Sekione Kitojo8 Desemba 2008

Katika uchaguzi mkuu nchini Ghana chama tawala NPP bado kinaongoza katika matokeo ya awali.

https://p.dw.com/p/GBWF
Eneo mojawapo la mji wa Accra kabla ya uchaguzi mkuu uliofanyika wiki hii.Picha: Stefanie Duckstein


►◄Chama tawala nchini Ghana New Patriotic party-NPP kimeendelea kuongoza katika kura zilizohesabiwa kufikia sasa za urais nchini Humo. Matokeo ya mapema katika maeneo bunge 18 yanaonyesha kuwa Nana Akofu Addo kutoka chama tawala anakaribu asilimia 54 ya kura zilizopigwa huku mpinzani wake John Evans Atta Mills akiwa na asilimia 44..


Kufikia sasa ni asilimia chache ya kura zilizohesabiwa huku matokeo ya uchaguzi huo mkuu yakitarajiwa katika muda wa siku tatu zijazo. Wachanganuzi wanasema ni vigumu kutabiri ni nani ataibuka mshindi kwani wagombea hao wawili wanakaribiana na huenda raundi ya pili ya uchaguzi huo ikifanyika tarehe 28 mwezi huu.


Ni idadi kubwa ya waghana waliojitokeza hapo jana-jumapili kushiriki katika uchaguzi huo wa kumchagua rais na wabunge. Hata hivyo hakuna visa vyoyote vibaya vilitokea licha ya tahadhari kuwa huenda kukatokea machafuko kama ilivyokuwa nchini kenya,zimbabwe na Nigeria mwaka huu baada ya kutangazwa kwa matokeo ya urais.


Uchaguzi huo unafanyika ili kuchukua nafasi ya John Kufor ambaye atalazimika kuondoka madarakani januari mwaka ujao baada ya kuhudumu kwa mihula miwili.Kufuor ameufufua uchumi wa Ghana kwa kuleta mabadiliko ya kiuchumi yaliyoelekezwa katika masoko na pia kuleta hali ya utulivu wa kisiasa. Kutokana na kuimarika kwa uchumi chama tawala New Patriotic Party-NPP kinaomba kupewa nafasi nyingine ili kuendelea na kibarua chake.


Hata hivyo licha ya uchumi huo ulioimarika,ukweli ni kuwa Ghana ndilo taifa la pili duniani linalozalisha zao la kakao kwa wingi na pia dhahabu, lakini umaskini umekithiri miongoni mwa waghana wa kawaida.


Vyama vyote viwili vimeahidi mabadiliko hasa linapokuja swala la mapato kutokana na mafuta yaliyogunduliwa nchini humo, na mradi huo unatajiwa kuanza mwaka 2010.

Uchaguzi huo uliwavutia wagombeaji Saba, huku sita wakijiondoa dakika za mwisho kama ilivyotarajiwa .Huu ni uchaguzi wa tano kufanyika nchini Ghana tangu kuanzishwa kwa vyama vya upinzani mwaka 1992.Nimeikamilisha mihula yangu miwili bila matatizo yeyote alisema rais Kufuor alipokuwa akipiga kura katika mji mkuu wa Ghana Accra.


Kuna Kinyanganyiro kikali kati ya chama tawala NPP na chama kikuu cha upinzani national Democratic Congress-NDC kilichokuwa madarakani mwaka wa 2000 wakati wa Jerry Rawlings.


Punde baada ya kupiga kura mgombea urais wa chama tawala Nana Akufo Addo alisema amefurahishwa na njisi uchaguzi huo ulivyoendeshwa. Akufo Addo mwenye umri wa miaka 64 ni wakili.


Mpinzani wa karibu wa Addo ni John Atta Mills mwenye umri wa miaka 64 na professor wa sheria. Wote wawili wametabiri ushindi.


Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi nchini humo anasema matokeo ya mwisho yanatarajiwa kuonyesha kuwa idadi kubwa ya waghana walijitokeza kushiriki katika uchaguzi huo mkuu.Matokeo ya muda yanatarjiwa kutolewa katika muda wa siku tatu,huku kukiwa na uwezekano wa raundi ya pili ya uchaguzi huo iwapo hata mgombea atakayepata asilimia 50 ya kura.














.