1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

GHANA-TOGO-I.COAST-ANGOLA NA TUNESIA KUWAKILISHA AFRIKA

10 Oktoba 2005
https://p.dw.com/p/CHYa

Kinyan’ganyiro cha kuania tiketi 31 kati ya zote 32 za Kombe lijalo la dunia nchini Ujerumani 2006 kiliuma mwishoni mwa wiki:Afrika ilijionea mapinduzi ya Kombe la dunia kwani, itawakilishwa mwakani nchini Ujerumani na timu 4 mpya:Angola,Togo,Ivory Coast na Ghana.Timu hizo zitakazojiunga na mabingwa wa Afrika Tunesia kukamilisha orodha ya timu 5.

Kufuatia changamoto za mwishoni mwa wiki kanda mbali mbali kuania tiketi 31 za Kombe lijalo la dunia Ujerumani, timu 13 zilikata jana tiketi zao.Kanda ya Ulaya, Uingereza,Itali na Holland ziliongoza njia zikifuatwa na Ureno,Croatia na Poland.hapo kabla tayari Ukraine na wenyeji Ujerumani walikwishapita.

Ujerumani ilipimana nguvu na Uturuki na kwa mara nyengine tena imeteleza ilipochapwa mabao 2:0 na Uturuki mjini Istanbul.Kikulacho kiko nguoni mwako.mabao 2 ya Uturuki yalitiwa na chipukizi 2 wa kituruki-wazaliwa wa Ujerumani na wanaocheza katika Bundesliga:Halil Altintop alieufumania kwanza malngo wa Ujerumani mnamo dakika ya 25 ya mchezo na Nuri Sahin,akapiga hodi mnamo dakika ya 89 ya mchezo. Sahin amekuwa mchezaji mchanga kabisa kucheza katika Bundesliga akiteremka uwanjani akiwa na umri wa miaka 16 alipoichezea Borussia Dortmund.

Katika kanda ya Amerika Kusini ,baada ya Argentina na Brazil ,jana zilifuata Paraguay na Ecuadaor.Costa Rica iliilaza Marekani na kunyakua nayo nafasi yake katika Kombe lijalo la dunia.Marekani kama Mexico, ilikwishachukua nafasi yake kwa Kombe lijalo la dunia.

Mapinduzi au zilzala ilizuka katika kanda ya Afrika-kwani timu 4 chipukizi na zisizo maarufu –Togo,Angola,Ivory Coast na Ghana zinashiriki kwa mara ya kwanza katika Kombe lijalo la dunia wakati simba wa nyika-Kameroun,Super Eagles-Nigeria,Senegal iliogonga vichwa vya habari mara iliopita,zimepigwa kumbo sawa na Morocco –timu ya kwanza ya Afrika katika Kombe la dunia 1970 .Badala ya Morocco inakuja Tunesia iliotoka nyuma mara 2 na kusawazisha mabao 2:2 na Morocco ili kushinda.

Msangao mkubwa ulizushwa na chipukizi Togo,kwani mara mbili ilitoka nyuma na mwishoe, kuwalaza simba wa Kongo na kuwapokonya tiketi wale wa Senegal.Kwa ufupi huu haukuwa mwaka wa simba-kwani si wa nyika, au wa Atlas wa Morocco wala wale wa Senegal walionguruma.Lakini ni mwaka wa Tembo wa Ivory Coast na nyota n yeusi-Black Stars-Ghana.Togo iliizaba Congo mabao 3-2 na mjini Lome ikawa shangwe na shamra-shamra.Rais wa Togo alitangaza leo ni siku ya mapumziko na chama cha upinzani kikawapongeza wanadimba wa Togo kwa kukata tiketi ya Kombe la dunia.

Angola ilitia bao la ushindi mnamo dakika 10 za mwisho dhidi ya Rwanda mjini Kigali.

Ghana iliikumta Cape Verde mabao 4:0.Msiba ulizikumba timu 2:Simba wa nyika Kamerun na Morocco:Kamerun ilikua njiani kuja Ujerumani baada ya Rudolph Douala kuipatia bao katika kipindi cha kwanza Mohamed Shawki akawaokoa waivory Coast aliposawazisha bao hilo.katika kipindi cha kufidia, simba wa nyika walipewa mchapo wa mkwaju wa penalty,lakini hawakuupokea.

Kwahivyo, ikawa tembo wa Corte d’ivore na sio simba wa nyika,wanaokuja Ujerumani mara hii.

Morocco ikiongoza bao 1:0 dhidi ya mabingwa wa Afrika Tunesia.Na baada ya wenyeji Tunesia kusawazisha,Morocco ilitangulia tena.Ikionekana kana kwamba, ni Morocco inayokuja Ujerumani, Tunisia ilisawazisha 2:2.

Maalfu ya watunesia wakaingia barabarani mjini Tunis na kwengineko nchini kushangiria wakati mjini Rabat,Morocco msiba ulitanda kama mapema mwaka huu pale Tunesia ilipoilaza Morocco mabao 2:1 katika finali ya kombe la Afrika la mataifa.Firimbi ya mwisho ilipolia,ilikua matanga nchini Morocco.Watu walijiinamia kwa huzuni.Huo ukawa ushindi mwengine mkubwa kwa kocha wa Tunesia,Mfaransa Roger Lemerre,alieiongoza Ufaransa kutwaa ubingwa wa Ulaya na halafu Tunesia wa Afrika na sasa ameipatia nafasi ya Kombe la dunia.

Timu zifuatazo zitashiriki katika finali ya Kombe lijalo la Afrika la Mataifa mjini Cairo,Misri ,Januari mwakani, Afrika Kusini,Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ni miongoni mwa timu hizo.Nyengine ni wenyeji Misri,Angola,Kameroun,Ghana,Guinea,Ivory Coast,Libya,Morocco,Nigeria,Senegal,Togo,Tunesia,Zambia na Zimbabwe.