1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghana na Mali zafuzu robo fainali

2 Februari 2012

Emmanuel Badu ameikatia Ghana tiketi ya mechi za robo fainali katika dimba la Mmataifa ya Afrika baada ya kufunga bao lililowasaidia kutoka sare ya goli moja dhidi ya Guinea hapo jana.

https://p.dw.com/p/13vFV

Mali pia walijiunga na Ghana kwa hisani ya bao lake la ushindi Seydou Keita dhidi ya Botswana. Kiungo wa kati wa Ghana Badu mwenye umri wa miaka 21 aliichukua pasi kutoka kwa mkwaji wa kona nje ya sanduku la lango, akauzungusha juu mpira kwa guu lake la kushoto kisha akasukuma kombora nzito hadi wavuni na guu lake la kulia na kuwapa Black stars pointi moja waliyohitaji.

Nalo bao la kwanza katika dimba hilo, lake mchezaji bora wa mwaka aliyemaliza wa pili mwaka jana Keita, katika dakika ya 75 liliipa Mali ushindi wa magoli mawili kwa moja dhidi ya Botswana wanaoshiriki kwa mara ya kwanza, ambao mchuano wao wa mwisho walizabwa magoli sita kwa moja na Guinea.

Ghana wanaongoza kundi D na pointi saba, huku Mali wakiwa wa pili na pointi sita nao Guinea wakiwa na nne. Botswana walishindwa kujikwamua. Michuano yote ya Ghana dhidi ya Guinea mjni Franceville na Mali dhidi ya Botswana mjini Libreville ilichezwa katika viwanja vilivyokuwa na upungufu wa mashabiki tatizo ambalo pia linalitatiza dimba hilo nchini Gabon ambako michuano hiyo ilichezwa jana, na pia kule kwa wenyeji wengine Guinea ya Ikweta.

Utovu wa nidhamu washuhudiwa

Kinyang'anyiro hicho kilikumbwa pia na tukio jingine la utovu wa nidhamu wakati kiungo wa kati wa Tunisia Abel Chedi alipojiondoa kutoka kikosini baada ya kushindwa kupata fursa yoyote ya kucheza katika dimba hilo. Chedli aliiwacha timu hiyo mjini Franceville na amerejea nyumbani kulingana na afisa wa habari wa Tunisia Zouhaier Ward.

Mudather Eltaib wa Sudan, kulia, na Charles Kabore wa Burkina Faso
Mudather Eltaib wa Sudan, kulia, na Charles Kabore wa Burkina FasoPicha: AP

Chedli, mzaliwa wa Ufaransa, ambaye alishinda kombe hilo mnamo mwaka 2004, alifurushwa hadi viti vya mashabiki wakati wa mchuano ambao Tunisia ilifungwa na wenyeji Gabon goli moja kwa bila, baada ya kulalamika kwa ghadhabu wakati alipowachwa nje ya kikosi kilichoucheza mchuano huo.

Kuondoka kwa Chedli, kabla ya mchuano wa Tunisia wa robo fainali siku ya jumapili unafuatia kutimuliwa kwa Mzambia Clifford Mulenga na timu yake kwa kukiuka sheria za muda uliowekewa wachezaji kurejea katika vyumba wanamoishi, na kisha akakataa kuomba radhi.

Ghana watakabana koo na Tunisia katika mchuano wa robo fainali siku ya jumapili huku Mali ikichuana na Gabon katika mojawapo ya michuano ya wazi nay a kusisimua katika dimba hilo kwa miaka mingi. Katika mechi nyingine jumamosi, wenyeji Guinea ya Ikweta watakutana na Cote d'Ivoire, ambao wanapigiwa upatu sana katika dimba hilo, pamoja na Ghana, na kisha Zambia itaumiza nyasi na Sudan.

Mashabiki wa Gabon
Mashabiki wa timu ya GabonPicha: AP

Ikiwa Guinea wangeshinda mchuano wao dhidi ya Ghana basi waandalizi wangelazimika kufanya hesabu ili kubaini timu mbili za kwanza kwa kutumia mbinu ya kutathmini takwimu za kila timu.

Kilio cha Guinea kupewa penalti kiligonga mwamba na bao lao lingine walilofunga likafutiliwa mbali kabla ya Badu, ambaye alikuwa katika kikosi cha Ghana cha wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20 kilichoshinda dimba hilo mwaka 2009 kuwaamsha mashabiki.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef