Ghana na Cote D'Ivoire zachukua nafasi zao halisi
2 Februari 2015Tukianzia katika kinyang'anyiro cha kombe la mataifa ya Afrika: Ghana na Cote D'Ivoire zimechukua fursa ya kukaa pale zinapostahili katika jukwaa la mataifa ya Afrika katika soka , baada ya kukata tikiti zao kuingia katika nusu fainali ya kombe la mataifa ya Afrika kwa kuzifungashia virago Guinea na Algeria kurejea makwao jana Jumapili wakati michuano hiyo ikirejea katika hali ya kawaida baada ya utata uliojitokeza katika michezo ya kwanza ya robo fainali siku ya Jumamosi.
Wilfried Bony hatimaye alionesha uhai , akiweka wavuni mabao mawili kwa kichwa upande wa Cote D'Ivoire , na bao la dakika za mwisho la Gervinho lilikamilisha ushindi wa kihistoria wa mabao 3-1 kwa Tembo hao wa Cote D'Ivoire wakati wakiingia katika nusu fainali kwa mara ya nne katika mashindano mara sita ya bara hilo.
Black Stars wa Ghana watakumbana na wenyeji wa mashindano Guinea ya Ikweta siku ya Alhamis na Tembo wa Cote D'Ivoire , ambao wamelinyakua mara moja tu taji hili barani Afrika mwaka 1992 kabla ya kuingia kile kinachojulikana kama "kizazi cha dhahabu",wanakutana na jamhuri ya kidemokrasi ya Congo mjini Bata siku ya Jumatano.
Nilizungumza na mwanamichezo wetu David Kwalimwa ambaye yuko hivi sasa mjini Malabo, ambapo kwanza nilitaka kujua tathimini yake ya michezo ya robo fainali na timu zilizoingia fainali, na pia matamshi ya kocha wa Cote D'Ivoire kwamba timu bora katika bara la Afrika Algeria imeshindwa. Yeye ana maoni gani.
Ni David Kwalimwa kutoka Malabo nchini Guinea ya Ikweta.
Kocha wa Algeria Christian Gourcuff amedai kuwa kikosi chake kilikuwa bora licha ya kushindwa kwa mabao 3-1 dhidi ya Cote D'Ivoire mjini Malabo jana Jumapili na kutolewa nje ya kinyang'anyiro hiki cha kombe la mataifa ya Afrika.
Sakho na West Ham United zachunguzwa na FIFA
Wakati huo huo shirikisho la kandanda duniani FIFA limesema leo limeanza uchunguzi dhidi ya mshambuliaji wa Diafra Sakho na klabu yake ya West Ham United ya Uingereza , kwa uwezekano wa kukiuka sheria za shirikisho hilo kuhusu kutoshiriki kwa mshambuliaji huyo katika kikosi cha Senegal katika michuano ya kombe la mataifa ya Afrika.
Sakho ameshindwa kujiunga na kikosi cha Senegal akidai kuwa ana maumivu ya mgongo lakini aliichezea timu yake ya West Ham dhidi ya Bristol City Januari 25 na kufunga bao la ushindi. Michuano ya kuwania kombe la Afrika ilianza Januari 17 na itafikia mwisho siku ya Jumapili na FIFA itatoa uamuzi wake Jumatatu ijayo.
Tukiiangalia sasa Ligi ya Ujerumani Bundesliga, Bayern Munich imepata kipigo chake cha kwanza msimu huu , na ni kipigo cha mbwa mwizi dhidi ya VFL Wolfsburg iliyoko katika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo kwa kuicharanga mabao 4-1 katika siku ya ufunguzi rasmi wa mzunguko wa pili wa ligi hiyo, baada ya mapumziko ya majira ya baridi.
Bayern Munich hata hivyo inatupia jicho kufuta kipigo hicho cha kudhalilisha na kurejesha katika hali ya kawaida kampeni yake msimu huu , ambapo kesho Jumanne itaingia uwanjani tena kupambana na Schalke 04.
Wolfsburg ilipunguza pointi za Bayern hadi nane siku ya Ijumaa na inatarajia kupunguza zaidi iwapo Schalke 04 itaendeleza pale Wolfsburg ilipoishia dhidi ya Bayern. Wolfsburg iliyoko katika nafasi ya pili ina matumaini ya kumjumuisha mshambuliaji wa pembeni kutoka Chelsea Andre Scherrle katika pambano lake kesho Jumanne dhidi ya Eintracht Frankfurt iwapo watapata saini ya mchezaji huyo kabla ya dirisha la uhamisho kufungwa leo usiku.
Borussia Dortmund ambayo ni makamu bingwa wa msimu uliopita imeambulia pointi moja siku ya Jumamosi baada ya kupata sare ya bila kufungana dhidi ya Leverkusen lakini inashika mkia wa ligi hiyo katika nafasi ya 18 ikiwa na pointi 16 kibindoni. Nuri Sahin mchezaji wa kati wa Borussia anaielezea hali hiyo.
"Tulikuwa na mpango maalum tulioandaa, na tuliutekeleza. Na hilo ni muhimu, kwamba hatukutabakia watulivu, na kwamba hatutavurugikiwa. Na kwa hiyo hilo lilikuwa muhimu hii leo. Ni kitu cha kawaida kwamba tungependa kupata pointi zote tatu, lakini dhidi ya Leverkusen inawezekana kupata sare."
Hamburg SV ilishindwa tena kufurukuta siku ya Jumamosi wakati ilipolambishwa mabao 2-0 na FC Kolon , licha ya kupata huduma ya mshambuliaji Ivica Olic ambaye amesajiliwa wiki iliyopita kutoka Wolfsburg. Olic anasema ilikuwa bahati mbaya sana kwao.
"Ni bahati mbaya, kwani katika nusu ya kwanza tulipata nafasi nzuri za kupata magoli. Ni bahati mbaya , Kwa kuwa naamini , kwamba katika wakati huo tulikuwa timu bora. Na nina hakika , kwamba tungepata bao hali ingekuwa nyingine kabisa. Ingewalazimu Koln kufanya juhudi kubwa zaidi , kuliko ilivyokuwa kwetu."
Augsburg iliishinda Hoffenheim kwa mabao 2-1 jana mjini Augsburg na kusogea hadi nafasi ya tano na mshambuliaji wa Hoffenheim Kevin Volland anadai Augsburg ni timu ngumu nyumbani.
"Kila wakati hapa tunakuwa na mchezo mgumu. Pamoja na hayo tulipata nafasi nyingi nzuri za kupata mabao hususan katika kipindi cha pili na kupata fursa ya kubadilisha matokeo. Tulishindwa kutumia nafasi za kushambulia kwa kushitukiza vizuri, katika kipindi cha kwanza tulifungwa mabao mawili pasipo na hatari kubwa , kitu ambacho hakikupasa kutokea na kwa hiyo kushindwa kwetu hapa ni sawa kabisa."
Kesho Jumanne, Bayern Inapambana na Schalke 04, Borussia Moenchengladbach inaisubiri Freiburg, Hannover itaoneshana kazi na Mainz 05, na Eintracht Frankfurt ina miadi ya VLF Wolfsburg.
Jumatano ni zamu ya Borussia Dortmund ikijaribu bahati yake dhidi ya Augsburg, Hoffenheim inaisubiri Werder Bremen, Bayer Leverkusen inakwenda mjini Berlin kupambana na Hertha BSC, na FC Kolon inatiana kifuani na VFB Stuttgart, wakati FC Paderborn inakabana koo na Hamburg SV.
Na katika ligi ya Uhispania La Liga timu mbili bado zinafukuzana wakati Real Madrid ikipata ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Real Sociadad , Villareal iliisumbua Barcelona , lakini hatimaye ilisalim amri kwa kipigo cha mabao 3-2.
Urais wa FIFA
Rais wa sasa Joseph Blatter na wagombea wengine watatu wanawania kiti cha urais wa shirikisho la kandanda duniani FIFA baada ya Jorome Champagne kuwa mtu wa pili kujitoa katika kinyang'anyiro hicho.
FIFA imesema katika taarifa leo kwamba Blatter, mwanamfalme wa Jordan Ali Bin Al Hussein, mchezaji bora wa mwaka wa zamani duniani Luis Figo kutoka Ureno na mchezaji wa zamani wa soka wa Uholanzi Michael van Praag wamependekezwa na vyama vyao vya kandanda kugombea wadhifa huo.
Kiongozi wa zamani wa FIFA Champagne wakati huo huo ameliambia shirika la habari la dpa ameshindwa kupata uungwaji mkono kutoka vyama vitano wanachama wa FIFA, akipata vitatu tu. Mfaransa mwenzake David Ginola alijitoa kwa sababu kama hizo mwishoni mwa juma.
Mapambano dhidi ya Doping
Serikali nyingi zaidi zinapaswa kupitisha sheria zitakazofanya kuwa ni uhalifu kosa la kutumia dawa za kuongeza nguvu misuli kwa wanamichezo, doping , na mabadilishano ya taarifa yanahitajika kuongezwa kati ya viwanda vya madawa na vyama vinavyopambana dhidi ya doping kwa kuwa madawa si tatizo tena la pekee katika michezo, ameonya rais wa shirikisho la kupambana na madawa ya kuongeza nguvu katika michezo duniani WADA Craig Reedie.
Katika taarifa , iliyopatikana na shirika la habari la Reuters , rais wa shirika hilo la WADA amesema madawa hayo yamesambaa kupindukia eneo la michezo.
Mwandishi: Sekione Kitojo/ rtre / afpe / dpae
Mhariri: Yusuf , Saumu