Ghala la silaha lateketea nchini Chad na kusababisha vifo
20 Juni 2024Mashuhuda waliokuwepo karibu na mkasa huo wamesema anga la eneo hilo liligeuka kuwa jekundu kutokana na milipuko na moto mkubwa uliozuka. Mitetemo mizito ilisikika pia kiasi umbali wa kilometa 7 na majengo mengi yalitikisika.
Janga hilo limetokea kwenye mtaa wa Goudji, eneo ambako kuna ghala kubwa la jeshi la kuhifadhi silaha. Eneo hilo ni karibu pia na uwanja wa ndege wa kimataifa wa mjini N'Djamena na kambi inayotumiwa na wanajeshi wa Ufaransa walioko nchini Chad.
Moto huo uliozuka wakati giza lilipoingia hapo jana uliwaka kwa saa kadhaa kabla ya baadaye kufifia na hadi majira ya mawio ulikuwa umezimika kabisa.
Rais Mahamat Idriss Deby wa Chad alitoa taarifa ya mkasa huo kupitia ukurasa wake wa Facebook akisema watu kadhaa wamekufa na wengine wamejeruhiwa kutokana na moto. Taarifa yake lakini haikutaja idadi ya vifo wala majeruhi.
Ameitumia vilevile kutuma salamu za pole na rambirambi kwa familia zilizopoteza ndugu na jamaa na kuwatakia afua ya mapema wale walipatwa na majeraha. Kiongozi huyo pia ameahidi kuanzisha uchunguzi mara moja kubaini chanzo cha moto huo.
Wakaazi wasimulia kilichotokea, serikali bado haijasema chochote
Mamlaka za nchi hazijatoa taarifa yoyote hadi sasa alau kueleza kwa uchache kile ambacho huenda kilisababisha moto na milipuko.
Wakaazi karibu na ghala hilo waliingiwa kiwewe, huku mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Oumar Mahamat akisema wengi walidhani milipuko iliyosikika ilikuwa ni mashambulizi ya kijeshi.
Mkaazi mwingine kwa majina ya Kadidja Dakou anayeishi maili chache kutoka ghala lilipo, amesema paa la nyumba yao limeng´oka kutokana na kishindo cha milipuko. Yeye na watoto wake watatu pamoja na majirani wengine walikimbilia barabarani kwa hofu kwamba nyumba zao huenda zingeporomoka.
Tangu moto ulipozima, polisi imeweka viziuzi vikali kuzunguka eneo la mkasa huo huku maafisa wengine wa usalama wakipita mitaani kuokota mabaki ya mabomu na silaha zilizoteketea.
Mkasa watokea katikati ya taharuki ya baada ya uchaguzi wenye utata
Katika kile kinachoonesha kwamba tukio hilo limesababisha vifo vya hadi makumi ya watu, mkaazi mmoja ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba serikali inafaa ijitokeze kuwasaidia. Amesema na hapa ninamnukuu "Familia nyingi zimefikwa na msiba na inatia huzuni" mwisho wa kunukuu.
Kwa sasa utawala mjini N'Djamena kupitia msemaji wake Abderaman Koulamallah umewarai watu kuwa watulivu.
Chad, taifa la watu milioni 18 na miongoni mwa yale masikini zaidi duniani, limekuwa kwenye hali ya taharuki kabla na baada ya uchaguzi wa rais wenye utata uliofanyika mwezi uliopita.
Uchaguzi huo ulimpatia ushindi wa asilimia 61 rais Mahamat Deby lakini upinzani na makundi ya kiraia yanasema uchaguzi huo ulijawa dosari zilizoutia doa.