1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghailani akutwa na kosa 1, afutiwa mengine 280

Admin.WagnerD18 Novemba 2010

Mahakama ya kiraia jijini New York yamuona mtuhumiwa wa ugaidi, Ahmed Ghailani, hana hatia kwa makosa zaidi ya 200 ya mauaji lakini ana hatia kwa kosa moja la njama ya mashambulizi dhidi ya mali za Marekani

https://p.dw.com/p/QCO7
Mchoro wa kesi ya dhidi ya Ahmed Ghailani
Mchoro wa kesi ya dhidi ya Ahmed GhailaniPicha: AP

Jumatano ya jana ilikuwa ni siku muhimu kwa historia ya kesi za ugaidi dhidi ya waliokuwa mahabusu wa jela ya kijeshi ya Guantanamo, Cuba, kwenye mahakama ya kiraia nchini Marekani.

Chini ya Jaji Lewis Kaplan, kwenye mahakama ya Lower Manhattan jijini New York, jopo la majaji 12 lilimtia hatiani Ahmed Ghailani kwa shitaka moja kati ya mashitaka 286 yaliyowasilishwa mahakani dhidi yake.

Ghailani, kijana wa Kitanzania mwenye miaka 36, na ambaye anaelezewa na vyombo vya habari kuwa mwenye uso wa kitoto, alikutikana na kosa moja tu la kupanga njama za kuharibu mali za Marekani, huku mashitaka mengine, kama yale ya kushirikiana na Al-Qaeda katika njama za kuwauwa raia wa Marekani katika mashambulizi ya mabomu yaliyouwa watu 224 huko Dar es Salaam na Nairobi yakitupiliwa mbali.

Hata hivyo, waendesha mashtaka wa serikali ya Marekani, wanaamini kwamba uamuzi huu wa jopo la majaji, bado hauondoshi uwezekano wa mtuhumiwa huyo kuhukumiwa kifungo cha maisha au kwa uchache miaka 20 jela.

Msemaji wa Idara ya Sheria ya Marekani, Matthew Miller, aliliambia Shirika la Habari la Ujerumani, DPA, kwamba serikali inaheshimu uamuzi wa jopo la majaji na inaridhika kwamba sasa Ahmed Ghailani atakabiliwa na hukumu inayomstahikia. Naye Muendesha Mashtaka Mkuu, Preet Bharara, alisema kwamba wataiomba mahakama impe kifungo cha maisha Ghailani katika hukumu yake iliyopangwa kutolewa Januari 25 mwakani.

Wakati wa uendeshwaji wa kesi hii iliyoanza mwezi mmoja uliopita, waendesha mashtaka walimtuhumu Ghailani kwa kupanga njama na kusaidia kuratibu mashambulizi dhidi ya balozi za Marekani. Lakini mawakili wake walisema kwamba mteja wao alighilibiwa na mawakala wa Al-Qaeda waliokuwa Afrika Mashariki kwa dhamira ya kuua Wamarekani. Ushahidi muhimu ambao ungelionyesha kwamba Ghailani anakiri makosa aliyotuhumiwa, ulikataliwa na mahakama kutokana na kuwepo kwa uthibitisho kwamba Ghailani aliteswa alipokuwa kwenye mahabusu ya siri ya Shirika la Ujasusi la Marekani, CIA, huko Pakistan wakati alipokamatwa mwaka 2004.

Wapangaji wengine wanne wa mashambulizi haya ya balozi ya Marekani mwaka 1998 wanatumikia vifungo vya maisha katika jela zenye ulinzi mkali nchini Marekani tangu walipohukumiwa mwaka 2001.

Mashambulizi haya ndiyo yaliyoleta taswira ya kiongozi wa Al-Qaeda, Osama bin Laden, kwa mara ya kwanza kwenye makini ya maafisa wa usalama wa Marekani na tangu hapo, yeye na msaidizi wake wa karibu, Ayman al-Zawahiri, wamekuwa wakihusishwa na mashambulizi mengine kadhaa ya kigaidi likiwemo lile la Septemba 11, 2001.

Kesi ya Ghailani ni ya kwanza ya watuhumiwa wa ugaidi waliokuwa wamezuiliwa kwenye kambi ya kijeshi ya Marekani iliyoko Guantanamo, Cuba, kusikilizwa katika mahakama ya kiraia, na ni mtihani wa kwanza kwa utawala wa Rais Barack Obama. Katika kampeni zake za mwaka 2004, Obama, ambaye binafsi ni wakili wa haki za kiraia, aliahidi kwamba angelihakikisha kuwa mahabusu wote walioko Guantanamo wanapelekwa kwenye mahakama za kiraia.

Pamoja na kuchelewa utekelezwaji wa ahadi hii, kesi ya Ghailani ni ushahidi kwamba hilo linawezekana.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DPAE

Mhariri: Yusuf Saumu Ramadhan