Gerd Müller ataka masoko wazi ya Ulaya kwa bidhaa za Afrika
10 Agosti 2018
Umoja wa Ulaya unaweza kuhimiza maendeleo na kuchangia kupunguza wimbi la wahamiaji kutoka Afrika kwa kuacha wazi moja kwa moja masoko yao kwa ajili ya bidhaa kutoka nchi hizo" matamshi hayo yametolewa na waziri wa misaada ya maendeleo wa serikali kuu ya Ujerumani Gerd Müller. "Fungueni masoko kwa bidhaa zote kutoka Afrika" amesema Gerd Müller katika mahojiano na gazeti la Die Welt, na kuongeza " Soko la Umoja wa Ulaya si wazi bado kwa bidhaa kutoka Afrika". Brussels ina uwezo wa kulipatia bara la Afrika cheo kipya ikiwa ni pamoja na cha kisiasa.
Katika daraja ya Umoja wa Ulaya Gerd Müller anashauri ateuliwe kamishna atakaeshughulikia masuala tofauti ya Afrika. Ametoa wito wa kuitishwa kwa muda maalum mkutano wa baraza la Umoja wa Ulaya na Afrika. Lakini kabla ya yote waziri wa misaada ya maendeleo wa Ujerumani anatilia mkazo suala la biashara ambapo bidhaa za Afrika ziruhusiwe kuingia bila ya kutozwa ushuru na bila ya kuwekewa kikomo katika soko la Ulaya.
Ujerumani inataka makubaliano mepya kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika
Gerd Müller, ambaye ni mwanasiasa wa kutoka chama cha Christian Social Union CSU, chama kidogo kutoka jimbo la kusini la Bavaria, mshirika wa jadi wa chama cha CDU cha kansela Angela Merkel anasema Ujerumani itakapokabidhiwa uongozi wa zamu wa taasisi ya maamuzi ya Umoja wa Ulaya, miaka miwili kutoka sasa, atahakikisha makubaliano mepya yanafikiwa kati ya Umoja wa ulaya na Afrika.
Hata hivyo masaa machache baada ya pendekezo la waziri Müller kutangazwa hadharani, wapinzani wake wa kisiasa wanalikosoa na kusema " linaficha ukweli".
Biashara huru na ya haki ni shida kufikiwa kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika
Mwenyekiti wa tume ya ushirikiano wa kiuchumi katika bunge la shirikisho Olaf in der Beck wa kutoka chama cha kiliberali cha FDP anasema "Müller anabidi aache kupiga porojo na badala yake atekeleze kivitendo anachosema", akimaanisha mpango aliotangaza nchini Ujerumani wa kuimarisha shughuli za kiuchumi barani Afrika ambao anasema umekuwa midomoni tangu miaka mitatu iliyopita.
Msemaji wa chama cha walinzi wa mazingira anaeshughulikia sera za maendeleo, Uwe Kekeritz anajiuliza kwanini Müller anaunga mkono hivi sasa mpango wa biashara huru kwa Afrika katika wakati ambapo yeye mwenyewe aliwahi kuunga mkono makubaliano ya Umoja wa Ulaya kupinga kufungulia masoko ya umoja huo kwa bidhaa za Afrika?
Roland Süss wa shirika linalopinga utandawazi Attac anahisi itakuwa shida kufikia biashara huru na ya haki kwa mabara haya mawili ikizingatiwa ile hali kwamba ,katika wakati nchi za Afrika zinapunguza ushuru kwa bidhaa kutoka ng'ambo nchi za Umoja wa Ulaya zinamimina bidhaa za bei rahisi barani humo na ambazo nyingi kati ya hizo zinafidiwa na Umoja wa Ulaya.
Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/dw.com
Mhariri: Josephat Charo