Genscher alivyoipa uhai Ujerumani mpya
30 Septemba 2014Ilikuwa ni majira ya kiangazi ya mwaka 1989. Wajerumani Mashariki walianza kuikana serikali yao, wakisaka hifadhi kwenye balozi za Ujerumani Magharibi nchini Poland, Hungary, Czechoslovakia na kwenye Ubalozi wa Kudumu wa Ujerumani Magharibi uliokuwa Berlin ya Mashariki. Kwanza walikuwa wachache tu, lakini punde wakafikia mamia na hatimaye maelfu, wote wakijaribu kupata ruhusa ya kuingia Ujerumani Magharibi.
Kwenye macho ya Wajerumani Magharibi, kitendo hicho kilikuwa halali, kwani kwa mujibu wa Sheria ya Msingi (Katiba), wote hao walikuwa Wajerumani. Wakati huo, Chama cha Wafanyakazi cha Kisoshalisti kilikuwa kinatawala nchini Hungary, na nchi ilikuwa imefilisika. Serikali mjini Budapest ilikuwa kwenye ukingo wa mabadiliko na kwa hivyo kukawa hakuna juhudi za kutosha kuulinda mpaka kati ya Hungary na Austria.
Mnamo tarehe 11 Septemba 1989, maelfu ya Wajerumani Mashariki wakaliangusha Pazia la Chuma lililokuwa halipenyeki. Walinzi wa mpakani wa Hungary hawakuwa na kubwa waliloweza kufanya kuzuia mmiminiko wa watu. Erich Honecker na serikali yake ya Ujerumani Mashariki waliogofywa, kama ilivyokuwa kwa maafisa wa serikali mjini Prague, ambao pia walichukulia kukaliwa kwa balozi kama kitendo haramu.
Lakini uamuzi wa pamoja ndani ya himaya ya Sovieti ulikuwa umeanza kutoweka. Kwenye majira ya mwisho ya kiangazi ya mwaka 1989, hakuna aliyeweza kujua upi maandamano hayo yangelifikia umbali gani. Hakuna hata mmoja, isipokuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Magharibi, Hans-Dietrich Genscher.
New York, 27 Septemba 1989
Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa ilitoa fursa ya kipekee kwa waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani na wenzake wa Umoja wa Sovieti, Ujerumani Mashariki na Czechoslovakia kujadiliana hali iliyokuwa ikizidi kuwa mbaya kwenye balozi. Mnamo tarehe 8 Septemba, raia 117 wa Ujerumani Mashariki walishawishiwa waondoke Ubalozi wa Ujerumani Magharibi uliokuwa Berlin Mashariki. Nyaraka za kuondokea hazikuwa sehemu ya makubaliano bali tu kinga ya kutoadhibiwa na kurejea makazini mwao.
Kuanzia hapo, Ubalozi huo ukafungwa, jambo lililoongeza shinikizo kwa balozi zilizoko Warsaw, Budapest na Prague. Maafisa wa serikali ya Ujerumani Mashariki walitarajia serikali ya Kansela Helmut Kohl ingelizifunga balozi hizo pia ili kutuma ujumbe madhubuti kwa wale waliotaka kuomba ukimbizi.
Lakini akiwa waziri wa mambo ya nje na mwenye dhamana ya balozi, Genscher alilikataa hilo moja kwa moja. Badala yake aliwaamuru wafanyakazi wa balozi hizo kuwafungulia milango Wajerumani Mashariki. Wakati huo huo, maelfu zaidi wakajazana kwenye balozi hizo tatu za Ujerumani Magharibi.
Mnamo siku ya Jumatano ya tarehe 27 Septemba 1989, Genscher alikula chakula cha jioni na mwenzake wa Ujerumani Mashariki, Oscar Fischer. Akatoa mapendekezo mawili: maafisa wa Ujerumani Mashariki wangeliweza kutoa viza za kutokea na kupiga muhuri paspoti kwenye balozi, au Wajerumani Mashariki wangelichukuliwa kwenda Magharibi ndani ya treni ambazo zingelipitia ndani ya Ujerumani Mashariki. Fischer alihitaji muda wa kujadiliana mapendekezo hayo na Honecker mwishoni mwa wiki. Kwa Genscher, muda huo angelikuwa amechelewa sana.
28 Septemba
Siku moja baadaye, Genscher na Fischer walizungumza kwa njia ya simu. Hali kwenye balozi – hasa kwenye ubalozi wa mjini Prague – bado zilikuwa tete. Fischer aliahidi kuyapeleka mapendekezo ya Genscher kwenye serikali ya Ujerumani Mashariki. Genscher aliomba pia msaada wa Waziri wa Mambo ya Nje ya Czechoslovakia, Jaromir Johanes, ingawa hakuahidi chochote.
Jioni yake, Genscher aliomba mkutano na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sovieti, Eduard Shevardnadze. Genscher aliambiwa aende ubalozi wa Sovieti, lakini hakuwa na gari. Hatimaye alipelekwa kwa gari ya polisi ya New York City, akiwa na ving'ora na vimulimuli. Kufika hapo tu, akamueleza Shevardnadze juu ya hali mbaya kwenye balozi zilizokaliwa. Shevardnadze aliuliza ikiwa watoto pia wamo kwenye sakata hili, ambapo Genscher alijibu “Wengi” naye Shevardnadze akaahidi kusaidia.
Jioni hiyo hiyo, Genscher alipata uungaji mkono wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, James Baker, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Roland Dumas.
Septemba 29
Genscher alikuwa njiani kuelekea uwanja wa ndege alipopata simu kutoka ofisi ya Fischer. Kulikuwa na taarifa muhimu inamgojea kwenye Ubalozi wa Ujerumani Mashariki mjini Bonn, alisema mtu aliyepiga simu, akiongeza kwamba “ni jambo la manufaa kuzungumza naye.“
Septemba 30
Kwenye ofisi ya Kansela mjini Bonn, Genscher na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani Magharibi, Rudolf Seiters, walifahamu kwamba Ujerumani Mashariki ilikuwa imekubaliana na pendekezo la pili kutoka kwa Genscher, yaani kuwaruhusu raia wa Ujerumani Mashariki wanaotaka kuondoka kupitia nchi hiyo wakiwa kwenye treni. Genscher akashinikiza zaidi kwa ajili ya kuwepo watu mashuhuri wa kuwasindikiza kama njia ya kujenda kuaminiana miongoni mwa raia wa Ujerumani Mashariki.
“Wakimbizi hawa hawawaaminini,“ alimwambia balozi wa Ujerumani Mashariki mjini Bonn, Horst Neubauer. Genscher na Seiters walipendekeza kwamba wao wenyewe ndio wawasindikize wakimbizi hao. Mwakilishi wa Ujerumani ya Mashariki mjini Bonn akaiarifu serikali yake na muda mfupi baadaye ruhusa ikatolewa.
Muda mfupi kabla ya Genscher na Seiter kuondoka kwenda Prague, Neubauer akawasiliana nao akiwaambia kuwa Ujerumani Mashariki imefuta ruhusa kwa watu hao wawili kusafiri na wakimbizi wa Ujerumani Mashariki. Wasiwasi ukaanza kuja juu.
Mkasa kwenye Kasri la Lobkowicz
Baada ya kuwasili kwenye ubalozi wa Ujerumani Magharibi mjini Prague, Genscher aliwasiliana tena na Neubauer. Ujerumani Mashariki ilikuwa imeng'ang'ania msimamo wake: kwamba maafisa wawili tu wa Ujerumani walikuwa wanaruhusiwa kwa kila treni.
Saa 12:58 magharibi, Genscher akajitokea kwenye kibaraza cha ubalozi wa Ujerumani Magharibi na kutamka kile ambacho kinaweza kuwa nusu sentensi maarufu kabisa kwenye historia ya karibuni ya Ujerumani: “Wapendwa Wajerumani wenzangu, tumekuja kwenu ili kuwajulisha kwamba leo, kuondoka kwenu….” Kilichobakia kikapokewa na kupotelea kwenye chereko chereko zilizozuka.
Saa 1:30 usiku, watu wa kwanza wakaondoka Kasri la Lobkowicz. Dakika tatu kabla ya hapo, shirika la habari la serikali ya Ujerumani Mashariki lilitangaza maelezo kutoka wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani Mashariki. Kwa sababu za kibinaadamu, serikali ilikuwa imeamua kuwafukuza watu wanaozikalia balozi za Ujerumani Magharibi kinyume cha sheria.
Saa 2:50 usiku, “treni la kwanza la uhuru” liliondoka Prague kuelekea Dresden. Mengine manne yakaondoka kwa kila baada ya masaa mawili kuelekea mji wa Hof, mpakani mwa Bavaria.
Kituo cha treni cha Hof, 1 Oktoba 1989
Saa 12:14 asubuhi, Wajerumani Mashariki 1,200 – wengi wao watoto – walifika kwenye kituo namba 8 katika kituo cha treni cha Hof. Kwa ujumla, watu 6,000 waliwasili Hof siku hiyo, wote wakiwa hawana paspoti. Maafisa wa Ujerumani Mashariki walikuwa wamezichukuwa kwenye treni. Walipokewa na umma mkubwa wa wasamaria wema na waandishi wa habari.
Wajerumani Mashariki wengine elfu kadhaa waliamua kuandamana kwa miguu na kuionesha serikali yao njia gani wimbi la mageuzi lilikuwa linaelekea. Wiki sita baadaye, Ukuta wa Berlin ukaanguka.
“Masaa yale machache kwenye ubalozi wa Ujerumani mjini Prague zilikuwa na nguvu sana kulikuwa nilivyowahi kufahamu,” alisema Hans-Dietrich Genscher akikukumbuka yaliyotokea. “Sote tulikuwa na la kufurahia.”
Mwandishi: Volker Wagener
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Josephat Charo