"Genscher alikuwa baraka kwa nchi yetu": Gauck
17 Aprili 2016Takriban watu 800 akiwemo Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani James Baker walihudhuria ibada hiyo ya mazishi iliofanyika katika Kituo cha Mikutano Duniani mjini Bonn uliokuwa mji mkuu wa zamani wa Ujerumani ya magharibi kabla ya kuhamishiwa Berlin kufuatia kuungana upya kwa Ujerumani mbili hapo mwaka 1990.
Akizungumza katika ibada hiyo ya mazishi Rais Joachim Gauck wa Ujerumani amesema "Genscher alikuwa mzalendo wa Ujerumani na alikuwa mtu aliyejitolea kwa Ulaya.Alikuwa baraka kwa nchi yetu."
Rais huyo ameongeza kusema ni vigumu kuifikiria Ujerumani bila ya Hans-Dietrisch Genscher
Amesema "kazi yake ya kupigania amani na uhuru ni dhamira kuu ya kazi yake ya kisiasa.Alikuwa na shauku kwa umoja wa Ujerumani halikadhalika umoja wa Ulaya."
Genscher alikuwa waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani aliyeutumikia wadhifa huo kwa muda mrefu kabisa nchini na alikuwa kiongozi muhimu katika historia ya baada ya kipindi cha vita nchini Ujerumani na barani Ulaya.
Mchango wa Gesncher huthaminiki
James Baker aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani wakati wa utawala wa Rais George W. Bush kuanzia mwaka 1988- 1992 aliuambia umma uliohudhuria ibada yake hiyo ya mazishi kwamba mchango wa Genscher wa muungano wa Ujerumani ulikuwa hauthaminiki.
Genscher kwanza alitumika kama waziri wa mambo ya nje kwa Ujerumani magharibi na baadae kwa taifa la Ujerumani lilioungana tena kwa jumla ya miaka 18 chini ya utawala wa Kansela Helmut Schmidt na Kansela Helmut Kohl.
Waziri wa mambo ya nje wa hivi sasa nchini Ujerumani Frank- Walter Steinmeir amesema kazi yake kubwa ilikuwa ni kukomesha kugawika kwa Ujerumani na kugawika kwa Ulaya.
Kufuatia kujitokeza kwa nyufa katika utawala wa mkono wa chuma wa Ujerumani Mashariki hapo mwaka 1989 na kuanguka kwa Ukuta wa Berlin Novemba 9 mwaka 1989 Genscher alikuwa mstari wa mbele katika juhudi za kuiungaisha Ujerumani Mashariki na Ujerumani ya Magharibi lengo ambalo lilifikiwa hapo tarehe 3 Oktoba mwaka 1990.
Cha kujifunza
Gesncher aliwahi kusema jibu kwa makosa ya historia ya Ujerumani na Ulaya ni Umoja wa Ulaya.Alitamka hayo wakati alipokuwa akitangaza kujiuzulu kutoka katika bunge hapo mwaka 1998.Alisema "Ni jibu kwa vita vibaya vya dunia.Sababu hizi zingalipo hadi leo hii."
Genscher pia alikuwa wazi katika kile ilichojifuza Ujerumani kutokana na unyama wa historia yake ya kale ya utawala wa Manazi.Ameandika katika wasifu wake wa kumbukumbu "Daima nimekuwa nikiona kwamba ni wajibu wa kizazi changu kuzuwiya marudio kwa matukio ya kipindi cha mwaka 1939 hadi 1945 nchini Ujerumani vitendo viliivyofanywa na Ujerumani." Ameendelea kuandika "Kazi hiyo itaendelea daima milele . Lazima tuzuwiye hata kuibuka kwa sera mpya za utaifa."
Genscher alizaliwa tarehe 21 mwezi wa Machi mwaka 1927 huko Reideburg karibu na mji wa mashariki wa Halle.Aliandikishwa katika jeshi la kawaida la Ujerumani katika miezi ya mwisho ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia ambapo alikuja kutekwa na vikosi vya Marekani hapo mwaka 1945 na kufungwa gerezani nchini Uingereza. Baada ya vita alisomea sheria katika Chuo Kikuu cha Leipzig lakini kutokana na kutokupendezwa na utawala wa kikomunisti wa Ujerumani Mashariki alikimbilia Ujerumani magharibi hapo mwaka 1952.
Mwandishi : Mohamed Dahman /DW/AP
Mhariri : Yusra Buwayhid