1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

GAZA:Hamas na Fatah wakubaliana upya kusitisha vita

16 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CC1b

Viongozi wa makundi hasimu ya Hamas na Fatah wamefikia makubaliano mapya ya kusitisha vita.Makubaliano hayo ni ya tatu katika muda wa saa machache..baada ya yaliyofikiwa kuvunjika baada ya muda mfupi kupita.Hatua hii inatokea baada ya siku ya mapigano katika Ukanda wa Gaza yaliyosababisha vifo vya watu 15.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu wa Palestina Ismail Haniye wa chama cha Hamas makundi hayo hasimu yameafikiana kuondoa wapiganaji wao japo haijulikani iwapo makubaliano hayo yatadumu.

Wapiganaji walimuua afisa mmoja wa serikali wa ngazi za juu wa Misri alipojaribu kuona iwapo makubaliano hayo yanadumishwa.Afisa huyo alipigwa risasi mkononi kwa mujibu wa afisa mmoja wa usalama wa Palestina alipotembea mjini akiandamana na Waziri mmoja wa Palestina,Ghazi Hamad wa Hamas pamoja na afisa mmoja wa Fatah.

Mapigano yaliendelea kwa saa moja baada ya Waziri Mkuu Ismail Haniye kutangaza makubaliano ya kusitisha vita.

Afisa huyo wa Misri alikuwa mmoja wa wapatanishi wanaojaribu kurejesha usalama katika eneo hilo.

Katika tukio jengine wapiganaji wa Hamas waliwauwa walinzi wanane wa Rais Mahmoud Abbas katika shambulio lililotokea kituo cha Karni cha Palestina kinalotumika kuingia Israel kwa mujibu wa duru za Fatah.Hamas kwa upande wao wanakanusha madai hayo na kulaumu Israel kusababisha vifo hivyo.Kwa mujibu wa Waziri wa Ulinzi wa Israel Amir Peretz nchi yake inajaribui kutojiingiza katika vita kwenye eneo la Gaza japo mashambulio mapya ya makombora yanashinikiza Israel kulipiza kisasi.

Vyama vya Hamas na Fatah viliunda serikali ya kitaifa miezi miwili iliyopita katika makubaliano yaliyofikiwa Saudia.Makubaliano hayo yanatatizwa na usimamizi wa jeshi la usalama jambo linalosababisha makundi yaliyojihami kwa silaha kuendelea na mapigano.