Gaza,Afghanistan na Ukraine Magazetini
13 Oktoba 2014Tuanze na mkutano wa wafadhili mjini Cairo.Gazeti la "Thüringische Landeszeitung" linaandika:"Kwa mara nyengine tena unaitishwa mkutano wa wafadhili.Bila ya shaka maafa yanayowasibu wakaazi wa Gaza hatuwezi kuyapuuza,lakini ni dhahir kwamba ni mashariki ya kati hasa ambako kwa miongo kadhaa sasa,hisia za chuki dhidi ya amani ni kubwa mno kupita kiu cha kutaka amani.Matokeo yake ndio yale yale,uharibu na maangamizi ambayo kila mara walipa kodi wa nchi nyengine ndio wanaolazimika kurekebisha.Mikutano ya wafadhili inatishwa kila mahala.Ni sawa lakini mbinu hizi nazo zinabidi zikome.Kwasababu wale ambao kila mara wanalazimika kutoa,wanachoka na wao kuona mabilioni yanayotolewa kwaajili ya ujenzi mpya wa miundo mbinu hayajasaidia chochote katika eneo hilo la maafa.Visa visivyokwisha vya chuki na kisasi vinabidi vikome sasa.
Gazeti la "Der neue Tag lina maoni sawa na hayo na linaandika:" Hata kama misaada iliyoahidiwa itaondowa vifusi vya maangamizi ya vita vya hivi karibuni huko Gaza,lakini machungu ya moyoni ya pande zote mbili,hayatopona kwa wepesi hivyo.Ili utulivu urejee katika ene hilo,mkutano wa wafadhili unabidi ufuatiwe na mkutano wa amani.Kwa bahati mbaya hakuna dalili kma mkutano huo utaitishwa hivi karibuni.
Eti Putin kweli anatafuta amani?
Mada nyengine iliyohanikiza magazetini ni kuhuu uamuzi wa rais Vladimir Putin kuwataka wanajeshi wa Urusi warejee nyuma toka eneo linalopakana na Ukraine.Ndo kusema kila kitu barabar?Gazeti la "Kieler Nachrichten" linaandika:
Nchi za magharibi zitafanya vizuri kama zitaendelea kuiangalia Moscow kwa jicho la wasi wasi.Kwasababu uamuzi wa Putin haumaanishi kama anaachilia mbali kufumba na kufumbua, ndoto yake ya kuwa na Urusi mpya katika eneo la mashariki ya Ukraine.Sawa kurejea nyuma wanajeshi ni dalili ya kutia moyo,dalili kwamba ufumbuzi wa amani unawezekana.Lakini haimaanishi hata kidogo kwamba Moscow inasalim amri.Ulaya ya mashariki Putin ana usemi na hilo halitobadilika.Anaweza wakati wowote ule kuwaauru wanajeshi wake warejee akiona mambo hayajamkalia vyema.
Afghanistan baada ya 2014
Mada yetu ya mwisho magazetini inahusiana na hatima ya Afghanistan baada ya mwaka 2014.Gazeti la "Lausitzer Rundschau" linaandika:"Mipango ya kuondolewa wanajeshi wa kimataifa wanaoongiozwa na NATO-Isaf hadi ifikapo mwisho wa mwaka huu wa 2014,isalie kama ilivyo.Lakini kwamba nchi hiyo iachwe peke yake,kuanzia mwisho wa mwaka 2016,kama vile nchi za magharibi zinavyopanga,hilo si jambo la maana kwa nchi hiyo.Shughjuli za tume za kutoa mafunzo na ushauri,zinabidi ziendelee kwa muda mrefu zaidi.Kansela Angela Merkel atabidi sio tu kumtanabahisha rais Obama kuhusu umuhimu uliopo,bali pia wananchi wa Ujerumani na familia za wanajeshi 800 watakaoendelea kuwepo nchini humo.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri:Yusuf Saumu