1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gaza. Majeshi ya Israel yaendelea kuishambulia Lebanon.

5 Agosti 2006
https://p.dw.com/p/CDOb

Majeshi ya anga ya Israel yamewauwa Wapalestina wanne , ikiwa ni pamoja na mpiganaji mmoja , kusini mwa Gaza leo asubuhi, wakati vikosi vya jeshi la nchi hiyo vinasogea karibu na kambi ya wakimbizi ikiwa ni sehemu ya mashambulizi yao dhidi ya wapiganaji.

Watu walioshuhudia wamesema kuwa kombora lililofyatuliwa na ndege za kijeshi za Israel liliangukia mbele ya nyumba moja katika mji wa Rafah, na kuwauwa watu wawili na kuwajeruhi wengine kadha wa familia moja , ambao walikuwa wakikimbia mashambulizi yanayozidi ya jeshi la Israel.

Wakati huo huo shambulio la anga karibu na mpaka wa kaskazini mashariki wa Lebanon na Syria limesababisha kiasi watu 26 kuuwawa na 20 wengine wamejeruhiwa. Maafisa wa eneo hilo wamesema kuwa makombora hayo yameshambulia shamba moja karibu na mji wa Qaa katika bonde la Bekaa na kwamba wahanga wote walikuwa ni wafanyakazi wa mashambani wa Syria.

Ndege za kivita za Israel pia zimepiga madaraja manne kaskazini ya Beirut, na kuzuwia upelekaji wa misaada ya kiutu katika eneo hilo.

Wakati huo huo mashambulio zaidi ya 150 ya ndege za kivita za Israel yamepiga maeneo ya kusini mwa Lebanon , na kuuwa watu saba. Nao wapiganaji wa Hizbollah wamerusha makombora 200 ndani ya Israel jana Ijumaa, na kuuwa watu watatu na kuwajeruhi wengi kadha. Makombora kadha ya Hizbollah yamefika katika mji wa Hadera, kiasi ya kilometa 80 kutoka mpaka wa Lebanon. Huu ni mji wa mbali zaidi upande wa kusini ambapo makombora ya Hizbollah yameweza kufika tangu mzozo huo kuanza wiki tatu zilizopita.