1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gattuso achukua mikoba ya AC Milan

27 Novemba 2017

Waliokuwa miamba wa Italia AC Milan wamemtangaza mchezaji wao wa zamani Gennaro Gattuso kuwa kocha wao mpya baada ya kumuonyesha mlango Vincenzo Montella

https://p.dw.com/p/2oKqI
Champions League - Gennaro Gattuso
Picha: picture-alliance/LaPresse/J. Moscrop

Mabingwa hao wa Ulaya mara saba wamemfuta kazi Montella baada ya kutoka sare ya bila kufungana na Torino hapo jana, matokeo ambayo yaliiacha katika nafasi ya saba kwenye ligi kuu ya kandanda Italia – Serie A. Gattuso mwenye umri wa miaka 39, aliichezea AC Milan mechi 450 kati ya 1999 na 2012, na akanyanyua Kombe la Dunia na Italia mwaka wa 2006. Tangu alipostaafu kucheza, amekuwa akifanya kazi na mfumo wa AC Milan kama kocha wa timu ya vijana

La liga

Valencia iliikaba Barcelona kwa sare ya bao moja kwa moja hapo jana katika ligi kuu ya kandanda Uhispania, La Liga, lakini walisaidiwa na marefarii wa mechi hiyo ambao walishindwa kuona bao la Messi katika kipindi cha kwanza. Messi alifunga bao baada ya mkwaju wake kutemwa na kipa wa Valencia na mpira ukavuka mstari wa lango katikati ya miguu yake lakini marefarii hawakuona. La Liga haijaanza kutumia teknolojia ya kuangalia kama mpira umevuka mstari wa lango au la. Sevilla walitoka nyuma na kuwazaba Villarreal 3-2. Sevilla wako katika nafasi ya tano, pointi mbili nyuma ya nambari nne Real Madrid na nambari tatu Atletico Madrid. Barcelona wako usukani na pengo la pointi nne wakifuatwa na Valencia na pointi nane mbele ya Atletico na Real.

Nchini England Manchester City watapambana na Southampton siku ya Jumatano wakilenga kuendeleza rekodi yao ya kutoshindwa mechi yoyote kati ya 18 katika mashindano yote msimu huu. Wana pointi 37 kati ya 39 kwenye Premier League. Manchester United, ambao wako nafasi ya pili na pengo la pointi nane, watachuana na Watford kesho Jumanne. Nambari tatu Chelsea wanawakaribisha Swansea Jumatano wakati nambari nne Tottenham wakicheza ugenini na Leicester. Arsenal katika nafasi ya tano wataangushana na Huddersfield wakati Liverpool katika nafasi ya sita wakipambana na Stoke.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri:  Mohammed Abdul-Rahman