Gari lagonga lango la ofisi ya Kansela Merkel
25 Novemba 2020Picha kadhaa zinalionesha gari hilo ambalo katika upande wake mmoja kumeandikwa ujumbe unaosema: ''Nyie wauaji wa watoto na wazee'' na ujumbe katika upande mwingine ukiwa umeandikwa kwa maandishi meupe ukisema: ''Acha Siasa na Sera za Utandawazi.''
Msemaji wa serikali ya Ujerumani, ameiambia DW kwamba gari hilo liligonga lango la kuingilia katika ofisi ya Merkel na kusababisha uharibifu kidogo. Kansela Merkel na watumishi wengine wa serikali na katika ofisi ya kansela hawakupata madhara yoyote.
Dereva anashikiliwa
Polisi wamesema bado wanamshikilia dereva wa gari hilo, lakini hawajatoa taarifa zaidi kuhusu mtuhumiwa huyo. Msemaji wa polisi mjini Berlin, Thilo Cablitz amesema wanaendelea kulichunguza tukio hilo kuona iwapo limefanyika kwa makusudi au limesababishwa na matatizo ya kisaikolojia.
"Asubuhi ya Jumatano majira ya saa nne kamili, mwanaume mwenye umri wa miaka 54 aliliendesha gari lake katika lango la ofisi ya kansela wa shirikisho. Tunachojua alikuwa analiendesha gari taratibu mno. Hivyo, madhara ni kidogo sana. Watu kwenye ofisi ya kansela, akiwemo Kansela wa Ujerumani wako salama. Hapakuwa na kitisho chochote," alifafanua Thilo.
Mwandishi habari wa shirika la habari la Ujerumani, DPA aliyekuwepo kwenye eneo la tukio, amesema mtu mmoja amejeruhiwa na anapatiwa matibabu kwenye gari la wagonjwa.
Ofisi ya kansela wa Ujerumani iliyoko mjini Berlin iko karibu na Ubalozi wa Uswisi pamoja na ofisi za bunge la Ujerumani. Lango la nje lililogongwa liko karibu na ofisi ya usalama nje ya jengo kuu na linaweza kuonekana na watu wanaopita mitaani.
Chanzo bado hakijajulikana
Hata hivyo, hakuna ishara iliyojionesha mara moja kilichosababisha tukio hilo, lakini limefanyika wakati ambapo Merkel alikuwa akifanya mkutano wa baraza la mawaziri na wakati akijiandaa kwa mkutano mwingine kwa njia ya video na viongozi wa majimbo 16 ya Ujerumani kuzungumzia iwapo waongeze hatua za kuzuia kuenea kwa virusi vya corona ambazo ziliwekwa Novemba 2.
Tukio la Jumatano linafanana na jingine lililotokea mwaka 2014, ambapo gari moja liligonga lango hilo hilo la kuingilia kwenye ofisi ya kansela, ingawa halikusababisha madhara yoyote. Gari hilo lilikuwa na ujumbe unaolaani mabadiliko ya tabia nchi na mwanaume mwenye umri wa miaka 48 alikamatwa. Haijafahamika mara moja iwapo tukio la mwaka 2014 linahusiana na tukio la leo.
Gari lililohusika katika tukio la Jumatano ni Volkswagen Sedan na lilikuwa na namba za usajili za mji wa Lippe, kutoka jimbo la North Rhine-Westphalia. Gari hilo linafanana na lile lililohusika katika tukio la 2014.
(AP, DPA, AFP, Reuters)