Gabriel aelezea matumaini katika mzozo wa Qatar na majirani
4 Julai 2017Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel anaendelea na ziara katika nchi za Ghuba ya Uarabu, katika juhudi za kusuluhisha mzozo mkubwa kati ya Qatar na nchi kadhaa za kiarabu zilizoiwekea vikwazo. Akizungumza muda mfupi uliopita katika Umoja wa Falme za Kiarabu, Gabriel ameelezea matumaini ya kupatikana suluhisho, akisema zipo njia nyingi za kuumaliza mzozo huo.
Waziri Gabriel amewasili katika Umoja wa Falme za Kiarabu akitokea Saudi Arabia, ambako jana alizungumza na waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo, kuhusu mzozo unaotokota kati ya Qatar kwa upande mmoja, na nchi nyingine nne za Kiarabu zilizoitenga kiuchumi na kidiplomasia. Akizungumza mjini Abu Dhabi, Gabriel amesema maoni yake yanafanana na yale ya Umoja wa Falme za Kiarabu, kwamba ufadhili wote kwa makundi ya kigaidi unapaswa kukomeshwa, na kuongeza kuwa zipo njia nyingi za kuumaliza mzozo kati ya Qatar na majirani zake.
Ufadhili kwa magaidi wafanywa na watu binafsi!
Baada ya mazungumzo na mwenzake wa Saudi Arabia Adel al-Jubeir hapo jana mjini Jeddah, Sigmar Gabriel nchi za eneo la Ghuba ya Uarabu zinaweza kunufaika kwa kukubaliana kuacha kuunga mkono ugaidi.
''Mtu akitafakari suluhisho bora linaloweza kupatikana kutokana na mzozo wa sasa, nadhani ni makubaliano kwamba kila upande uache kuunga mkono makundi ya kigaidi na yenye misimamo mikali'', amesema Gabriel na kuongeza kuwa ingawa inafahamika kuwa uungaji mkono huo haufanywi na serikali, bali mara nyinyi unafadhiliwa na watu binafsi, lakini eneo zima linapaswa kumaliza kabisa ufadhili kwa makundi yote hayo.
Waziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu Sheikh Abdullah bin Zayed al-Nahayan amesema nchi yake na washirika wake bado wanasubiri jibu kutoka upande wa Qatar, kuhusu masharti iliyotakiwa kuyatekeleza ili iweze kuondolewa vikwazo ilivyowekewa.
Sheikh Al-Nahayan amesema bado ni mapema kuzungumzia vikwazo zaidi kwa Qatar, akisisitiza hatua zaidi zitategemea jibu kutoka kwa wale aliowaita ''Kaka zetu wa Qatar''.
Qatar yakataa kuyumbishwa
Nchi za kiarabu zilizoungana kuiwekea vikwazo Qatar ambazo ni Saudi Arabia, Bahrain, Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu, hapo jana zilirefushwa muda wa mwisho kwa Qatar kwa saa 48, ili kuwaruhusu maafisa wa nchi hiyo kufikisha majibu kwa njia ya barua, kwa mfalme wa Kuwait ambaye amejitwisha jukumu la upatanishi.
Miongoni mwa masharti magumu iliyotakiwa kuyatekeleza mara moja Qatar ni kukifunga kituo cha televisheni cha al-Jazeera ambacho inakifadhili kifedha, kupunguza mahusiano na Iran, na kukiondoa kituo cha kijeshi cha Uturuki kwenye ardhi yake.
Hapo jana waziri wa mambo ya nje wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al-Thani alisema masharti hayo ya washirika wao wa zamani yatakataliwa. Vile vile wakili wa Qatar aliyaita masharti hayo ukiukaji wa sheria za kimataifa, akiyalinganisha na uonevu ambao kihistoria uliishia katika uhasama na vita.
Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe, rtre
Mhariri:Yusuf Saumu