1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gabriel hakupokea simu yangu-Netanyahu

28 Aprili 2017

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema alijaribu kumpigia simu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel, ila Gabriel alikataa kupokea simu.

https://p.dw.com/p/2c4Cp
Israel Benjamin Netanjahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: picture-alliance/dpa/J. Büttner

Netanyahu alisema alikuwa amepiga simu kwa ajili ya kusafisha hali mbaya baina yao baada ya kufutilia mbali mkutano wake na waziri huyo alipoizuru Israel.

Netanyahu alifutilia mbali mkutano wake na Gabriel Jumanne wiki hii, baada ya waziri huyo wa nchi za nje wa Ujerumani kukutana na makundi ya kutetea haki za kibinadamu yanayoishutumu serikali ya Israel kwa jinsi inavyowanyanyasa Wapalestina.

Mzozo huo huenda ukaongeza mgawanyiko uliopo baina ya Israel na Ujerumani kuhusiana na suala la Palestina. Ujerumani imekuwa ikizishutumu sera za serikali ya Netanyahu za kujenga makaazi katika eneo ambalo Wapalestina wanataka taifa lao na hata nchi zenye ushawishi mkubwa duniani zinasema jambo hilo litachangia katika kuhujumu mipango ya amani.

Gabriel alikutana na makundi ya haki za kibinadamu Israel ikiadhimisha Holocaust

Na sasa Netanyahu alipokuwa akizungumza na gazeti mashuhuri la hapa Ujerumani, Bild, alisema, "nilimpigia simu bwana Gabriel na nieleze msimamo wangu ili kuweka mambo sawa, ila hakupokea simu, natumai Gabriel atakutana na mimi katika ziara yake ijayo ya Israel badala ya kukutana na makundi madogo yaliyo na misimamo mikali na yanayohujumu usalama wa Israel."

Israel Yad Vashem Gedenken
Viongozi wa Israel katika maadhimisho ya Holocaust 24.04.2017Picha: picture-alliance/Newscom/A. Cohen

Waziri mkuu huyo wa Israel anasema, Gabriel alikutana na makundi hayo katika siku ambayo nchi yake ilikuwa inaadhimisha mauaji ya halaiki ya Wayahudi ya Holocaust. "Hizi ndizo siku tunazoomboleza kuuwawa kwa wanajeshi na wananchi wetu katika Holocaust. Jeshi la Israel ndiyo nguvu inayowaweka watu wetu salama leo," alisema Netanyahu.

Baada ya mkutano huo baina ya Gabriel na Netanyahu kufutiliwa mbali, waziri huyo wa nchi za nje wa Ujerumani alisema suala hilo haliashirii kuvunjika kwa uhusiano baina ya nchi hizo mbili, kwani watapata nafasi nyengine ya kuzungumza kupitia simu au hata kukutana.

Ujerumani imekuwa makini katika mahusiano yake na Israel

"Lakini uhusiano wangu na Israel na uhusiano wa Ujerumani na Israel hautobadilika kwa njia yoyote kutokana na hilo, sisi ni nchi mbili tunaoshirikiana kwa karibu sana," alisema Gabriel.

Außenminister Gabriel in Israel
Waziri wa nchi za nje wa Ujerumani Sigmar GabrielPicha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Kutokana na jukumu lake la kihistoria la kuhusika pakubwa katika mauaji ya Wayahudi milioni sita katika Holocaust, Ujerumani imekuwa sio tu rafiki mkubwa wa Israel, bali pia imekuwa makini sana katika mahusiano yake na nchi hiyo ya Mashariki ya Kati.

Gabriel ambaye amewahi kuzungumza wazi kuhusiana na uhusiano uliovunjika na baba yake ambaye alishabikia Unazi, alikuwa ameizuru kanda ya Mashariki ya Kati ili kutafuta suluhu katika mzozo wa Israel na Palestina.

Mwandishi: Jacob Safari/Reuters/AFPE

Mhariri: Mohammed Khelef