1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

G7 yaionya Urusi kuhusu mzozo wa Ukraine

5 Juni 2014

Viongozi wa kundi la nchi saba zilizostawi kiviwanda ulimwenguni, wanakutana mjini Brussels bila kumwalika Vladmir Putin, na wamemtaka rais huyo wa Urusi autulize mzozo wa Ukraine, au akabiliwe na vikwazo vipya

https://p.dw.com/p/1CCa8
G7 Gipfel Brüssel Gruppenfoto 05.06.2014
Picha: Reuters

Hayo yanajiri wakati Rais Putin akitarajiwa kukutana na baadhi ya viongozi hao kwa mara ya kwanza tangu Urusi ilipolichukua rasmi jimbo la Crimea. Viongozi wa nchi za kundi la G7 walitoa taarifa ya pamoja baada ya mkutano wao jana jioni, wakiitaka Urusi ichukue hatua madhubuti za kuutuliza mgogoro wa mashariki mwa Ukraine, au iwekewe vikwazo zaidi.

Kansela wa Ujerumani aliuambia mkutano wa waandishi wa habari kuwa nchi za Magharibi zitatathmini kwa mara nyingine kuona hatua zitachukuliwa za kuituliza hali mashariki mwa Ukraine. Merkel alisema "Kundi la G7 limeshikilia msimamo wa wazi katika wiki za karibuni kuhusu suala la Ukraine na Urusi. Tutatafakari namna ya kuisaidia Ukraine baada ya uchaguzi wa rais, pili, tutaendelea na mazungumzo na Urusi kisha hatua mwafaka zichukuliwe, na tatu iwekwe wazi kuwa kama hakuna kitakachofanyika basi tutaamua kuhusu vikwazo vipya"

Rais wa Ufaransa Francois Hollande – ambaye anatarajiwa kuwa na mikutano miwili tofauti ya chakula cha jioni na Putin na Obama mjini Paris hii leo – amekubali kuwa mazungumzo pamoja na kutulizwa mzozo ni mambo ambayo lazima yahimizwe.

Belgien G7 Gipfel in Brüssel 04.06.2014
Mkutano wa G7 umeandaliwa kwa mara ya kwanza katika miaka 17 bila kuishirikisha UrusiPicha: Reuters

Rais Putin alidokeza kuwa huenda akakutana na Poroshenko na hata Obama, akisema kuwa hapangi kumwepuka yeyote. Masharti ya G7 ni pamoja na kuitaka Urusi ishirikiane na rais mpya wa Ukraine Petro Poroshenko na ichukue hatua za kusitisha usambazaji wa silaha na wanaharakati wanaopigania kujitenga katika mpaka wa Urusi. Hatua za kukata usambazaji wa gesi pia zinasemekana kujumuishwa.

Viongozi kutoka Marekani, Ujerumani, Ufaransa, Canada, Uingereza, Japan na Italia walishiriki katika mazungumzo hayo ya mjini Brussels. Kutokuwepo kwa Putin kulidhihirika wazi, hasa kwa sababu Urusi ndio inayoshikilia uwenyekiti wa kundi la G8 katika mwaka huu wa 2014.

Viongozi wa kundi hilo walipiga kura mwezi Machi kusitisha uwanachama wa Urisi na kuliita kundi hilo G7, kama hatua ya kujibu kitendo cha Urusi kulifanya jimbo la Crimea kuwa sehemu ya himaya yake.

Kumbukumbu ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia

Licha ya Urusi kutengwa katika mkutano wa G7 mjini Brussels, Putin anatarajiwa kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na Merkel, rais wa Ufaransa Francois Hollande na Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron katika kumbukumbu ya miaka 70 ya uvamizi uliofanywa na wanajeshi wa washirika katika eneo la Normandy wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Viongozi hao wa G7 pia wamesema wataungana dhidi ya kitisho cha ugaidi barani Ulaya kinacholetwa na wapiganaji wa itikadi kali wanaorejea kutoka vitani nchini Syria. Kundi hilo linakamilisha mkutano wao leo kwa kuangazia mada kama vile matumizi ya gesi barani Ulaya pamoja na mabadiliko ya tabia nchi na muafaka unaopendekezwa wa biashara baina ya Umoja wa Ulaya na Marekani.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Josephat Charo