Serikali ya muungano ya mrengo wa shoto
8 Juni 2015Tuanzie lakini Elmau ambako mkutano wa kilele wa viongozi wa mataifa saba tajiri zaidi kiviwanda duniani umeingia siku yake ya pili na ya mwisho hii leo.Mataifa saba na sio manane,kwasababu Urusi ya Vladimir Putin haikualikwa kwasababu ya mzozo wa Ukraine.Gazeti la "Lausitzer Rundschau" linaandika:"Kama kweli mkutano wa G7 bila ya Urusi una thamani ,hilo litadhihirika matokeo ya mkutano huo wa viongozi wa taifa na serikali yatakapotangazwa baadae leo hii.Angela Merkel,Barack Obama na washiriki wengine wa G7 wamemwambia wazi kabisa Vladimir Putin,mlango wa kuingia katika meza ya majadiliano ya vigogo wa dunia,umefungwa kwasababu ya uchokozi wa Urusi nchini Ukraine.Atakaeilamu G7 kutopima ipasavyo kwa kutafuta mvutano pamoja na Urusi,anakosea.Katika serikali ya muungano inayoongozwa na kansela Merkel mjini Berlin,manung'uniko yamehanikiza.Ni sawa kabisa kwamba katika siasa za kimataifa mengi hayawezekani bila ya Urusi,lakini na bila ya China.Na hilo Merkel analijua na Obama pia.Lakini ukweli ni kwamba Urusi yenyewe ndiyo yenye uwezo wa kuufungua mlango wa G7.Kwa kufuata siasa ya aina nyengine na kurejea kufuata misingi ya kuelewana na ushirikiano wa amani.
Uwezekano wa serikali ya muungano wa mrengo wa shoto
Mwenyekiti mashuhuri wa chama cha siasa kali za mrengo wa kushoto,Greogor Gysi anasema hatogombea tena wadhifa huo msimu wa mapukutiko mwaka huu.Uamuzi huo unaweza kufungua njia ya kuundwa serikali ya mungano ya vyama vya mrengo wa kushoto katika daraja ya taifa.Gazeti la "Volksstimme" linaandika:"Gregor Gysi hawezi kulinganishwa na kiongozi yeyote yule mwengine wa die Linke anaejiuzulu.Amekuwa kitam,bulisho cha chama cha siasa kali za mrengo wa kushoto kwa muda wa miaka 25 sasa nchini Ujerumani.Uhasama sawa na sifa amejikusanyia-Gysi amemeza na kujivunia mengi.Kujiuzulu kwake ni pigo kwa chama chake.Gysi ni mshika bendera wa die Linke,anapendelea mageuzi badala ya mapinduzi.Na hilo amelishadidia katika mkutano mkuu wa chama chake mjini Bielefeld.Chama kikitilia manani aliyoyasema-hali hiyo inaweza kufungua njia ya kuundwa serikali ya muungano pamoja na vyama vya SPD na walinzi wa mazingira die Grüne,uchaguzi mkuu utakapoitishwa mwaka 2017.Nafasi ya hilo kufanikiwa inapungua kwa kujiuzulu Gysi.Mrengo wa kushoto wa die Linke ambao hauko tayari kukiridhia chama cha SPD unapata nguvu.Wanaoshangiria ni CDU/CSU wanaozidi kujiimarisha.
Mkutano wa amani ya dunia
Mkutano mkuu wa kanisa la kiinjili umemalizika jana mjini Stuttgart.Zaidi ya waumini laki moja wameshiriki katika sherehe na ibada ya kuufunga mkutano huo.Gazeti la "Stuttgarter Nachrichten "linaandika:"Ulimwengu unazidi kuwa wa shida-na hilo limedhihirika katika mkutano mkuu wa kanisa la kiijili."Mkutano mkuu wa amani"uliokuwa ukizungumziwa tangu mwanzo,umesalia jina licha ya maazimio yaliyopitishwa.Hata hivyo hakupita bure-mada kadhaa zilizingatiwa kuanzia masuala ya usawa katika jamii,kupitia ndowa ya watu wa jinsia moja mpaka kufikia uhamiaji na sera kuhusu wakimbizi.Na yaliyojadiliwa yamewaingia walioshiriki,kitu ambacho ni nadra kutokea hasa wakati huu ambao kila mmoja anashughulikia yale tu."
Mwabdishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri:Yusuf Saumu