G20: Mkutano wa kilele kujadili mazingira na Covid-19
30 Oktoba 2021
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, rais wa Marekani Joe Biden, rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson ni miongoni mwa viongozi hao. Rais wa China Xi Jinping ambaye hajasafiri nje ya nchi yake tangu kuzuka kwa janga la Covid-19, atashiriki kwa njia ya vidio.
Soma zaidi: Rais Joe Biden akutana na Papa Francis
Waziri mkuu wa Italia Mario Draghi anawapokea viongozi wanaowasili katika jengo la mikutano la kisasa lijulikanalo kama 'Nuvola', ikimaanisha mawingu, katika kitongoji cha kusini mwa mji wa Roma kilichojengwa na fashisti Mussolini.
Changamoto ya mazingira na janga la corona
Viongozi hawa wanakabiliwa na shinikizo la kutafuta suluhisho linalofaa kushughulikia kadhia ya mabadiliko ya tabianchi, kuelekea mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuongezeka kwa joto duniani, utakaofanyika mjini Glasgow, Scotland kuanzia Jumapili.
Soma zaidi: Mawaziri wa fedha na afya wa G20 wakutana mjini Roma
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ambaye pia yuko mjini Rome, ameonya kuwa mkutano huo unaweza kuambulia patupu, ikiwa nchi wachafuzi wakubwa wa mazingira hazitaweza kuondoa tofauti miongoni mwao, na kati ya nchi hizo na zile zinazoendelea.
Baada ya kuwasili mjini Roma, waziri mkuu wa Uingereza, Boris Johnson amesema nchi yake itachangia dozi milioni 20 za chanjo ya virusi vya corona ya AstraZeneca kwa nchi zinazoendelea, kama sehemu ya juhudi za kugawana chanjo na nchi ambazo hazijapata chanjo hiyo.
Soma zaidi: Mawaziri wa Mambo ya Nje na Maendeleo wa nchi za G20 wakutana nchini Italia.
Johnson amezitaka nchi zenye uchumi mkubwa za G20 kuhakikisha ulimwengu wote umepata chanjo ifikapo mwishoni mwa mwaka 2022, na kuongeza kuwa kipaumbele cha kwanza cha G20 kinapaswa kuendelea na usambazaji haraka wa chanjo ulio sawa na wa kimataifa.
Papa Francis aalikwa kuzuru India
Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi ametumia fursa ya ziara yake mjini Roma kumualika kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis kuizuru India. Mwaliko huo ameutoa baada ya kukutana na Papa Francis kwa mara ya kwanza.
India nchi yenye waumini wengi wa Kihindu, ina takriban Wakristo milioni 28. Kabla ya mkutano wa viongozi hao wawili, redio ya Kanisa Katoliki iliripoti kuwa maombi ya awali yaliyotolewa na Vatican kutaka Papa aizuru India, yalikataliwa na nchi hiyo.
afpe, rtre, ape