1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

G-8 na hali ya hewa

9 Julai 2008

Azimio juu ya hali ya hewa kutoka dola 8-tajiri (G-8) na ziara ya Obama Berlin-ni mada zilizotia fora leo.

https://p.dw.com/p/EZ9f

Uchambuzi wa wahariri wa magazeti ya leo ya Ujerumani, umetuwama juu ya maafikiano yaliofikiwa kwenye mkutano wa kilele wa dola 8 tajiri ulimwenguni (G-8) huko Japan kuhusu kutunza hali ya hewa.Pia masharti mapya ya uraia wa Ujerumani, yamechambuliwa na hata ziara ya mtetezi wa kiti cha Urais wa Marekani mjini Berlin, Seneta Barack Obama.

Maafikiano yaliofikiwa juu ya kuzuwia kuchafuka zaidi kwa hali ya hewa si makubwa tena kutokana na sababu kadhaa:Kwanza, laandika gazeti, rais Bush anaeondoka karibuni madarakani hataweza kutekeleza ahadi alizotoa.

Kuregeza kidogo kamba alikofanya Bush ,ni kumrahisishia tu jukwaa la kampeni ya uchaguzi wa urais mwenzake wa chama cha Republican John Mccain na kuonesha kana kwamba hata rais kutoka chama cha Republican anaungamkono jitihada za kulinda mazingira.

Pili, laendelea Kölnische Rundschau kuandika- Marekani inaendelea zaidi kukwepa jukumu lake la kuchangia kuzuwia uchafuzi wa mazingira kwa kadiri China na India hazitoi mchango wao.

India na china zinaelewa kwamba utoaji moshi unaochafua mazingira kwa kila mkaazi nchini Marekani ni kubwa mara 6 kuliko kwao.

Na tatu lamaliza gazeti, ikiwa yale mapatano ya Kyoto ya kimataifa hayana nguvu tena ,iweje maafikiano haya mapya ya heshimiwe ?

Mwaka 2009,lamaliza gazeti- ni zamu ya kopenhagen,kwa mkutano mwengine wa hali ya hewa...

Likiendeleza mada hii,gazeti la Westdeutsche Zeitung,laandika:

"Katika mkutano huo wa hali ya hewa hapo mwakani,nchi za kiviwanda zitapaswa kuamua wapi zinasimama: Ama zitabidi kuweka shabaha ya kuchukua hatua kali tena na mapema au nchi zinazostawi mno kiuchumi wakati huu-China na India,zitazipa mgongo zitapotakiwa kutoa mchango wao mwengine kuhifadhi mazingira.

Haiystahiki kuzilaumu nchi hizi.Kwani, mhindi anachafua mazingira kwa moshi unaopaa hewani kwa kima cha kilogramm 900 kwa mwaka wakati mjerumani ni kiligramu 10.000.

Nalo gazeti la OLDENBURG: Volkszeitung linatumalizia mada hii kwa kuandika :

Wakati unapita ikiwa tunataka kuhifadhi uchafuzi zaidi wa hali ya hewa na dola kuu zenye nguvu duniani zinakwenda mwendo wa konokono.Kwani, zaidi ya kuelezea nia ya kusonga mbele , hakua zaidi kilichopatikana kutoka kikao cha jana cha mkutano wa kilele wa mataifa 8 tajiri ulimwenguni nchini Japan....lasema gazeti.

Likifungua pazia kwa ziara ya Berlin,Ujerumani ya mtetezi wa wadhifa wa urais wa Marekani kwa tikiti ya chama cha Democrat Barack Obama,gazeti la Rhein-Zeitung kutoka Mainz laandika:

Serikali ya Ujerumani mjini Berlin, itafanya vyema ikiwa haitomruhusu Obama kuhutubia mbele ya Lango la Brandeburger Tor.

Hata ikiwa wajerumani wengi tayari wameshamtawaza Obama kitini kuwa ndie rais mpya wa Marekani au wangependa iwe hivyo,alama hiyo ya utambulisho wa wajerumani isigeuzwe jukwaa la kampeni ya uchaguzi wa rais .John McCain,mpinzani wake Obama na wafuasi wake wa chama cha republican wamestahiki kukereka kuona Obama anatiwa jeki namna hivyo mjini Berlin.

Mwishoe, gazeti la Westfälischer Anzeiger linauchambua mtihani wanaopaswa kufanyiwa wageni kutoka sasa wanaomba uraia wa Ujerumani.Laanidika:

Kuna kasoro nyingi katika orodha ya waziri wa ndani Bw.Schaüble:Maswali mengi ama hayafai au si wazi.

Katika maswali mengi yanayopaswa kujibiwa katika orodha ya maswali hata wajerumani-wazawa hawatapasi mtihani.

Ni barabara uraia usitolewe ovyo-ovyo au kirahisi, lakini sio kwa namna hii ilivyopangwa.Orodha za maswali ya kujibiwa zimetungwa na wataalamu,zimeandaliwa na wamangi-meza na hazilingani kamwe na hali hasa za kimaisha."

Lamaliza Westfälischer Zeitung.