Frankfurt yashinda kombe la shirikisho la Ujerumani
19 Mei 2018Eintracht Frankfurt imeshinda kombe la shirikisho la Ujerumani, DFB Pokal kwa kuikandika Bayern Munich 3-1 katika mechi ya fainali iliyochezwa leo katika uwanja wa Olympiastadio mjini Berlin. Pichani Ante Rebic akiufumania wavu wa Bayern kwa mara ya pili. Bao la tatu limefungwa na Mijat Gacinovic sekunde za lala salama. Frankfurt imechukua kombe hilo kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 30 na kama washindi wamefuzu moja kwa moja kucheza katika kombe la ligi ya Ulaya, Europa League, msimu ujao.
Rebic alianza kufunga dakika ya 11 na kufunga bao la pili dakika nane kabla dakika 90 kukamilika, baada ya refa wa video kuthibitisha bao lake alilifunga kwa haki. Katika sekunde za lala salama muda wa dakika nne za ziada Mijat Gacinovic alitimka mbio kama mshale na kuufumania wavu huku mlinda lango wa Bayern Munich Sven Ulreich akijisahau kabisa baada ya kuondoka langoni pake kwenda kuwasaidia wenzake katika kona waliyokuwa na matumaini ya kusawazisha na kuulazimisha mchezo uingie katika muda wa ziada. Frankfurt imelitwaa kombe la DFB Pokal kwa mara ya kwanza tangu mara ya mwisho walipolishinda mwaka 1988.
Juhudi za Bayern hazikufua dafu
Robert Lewandowski alifaulu kukomboa baada ya kipindi cha mapumziko, lakini Bayern Munich, ambao ni mabingwa wa ligi kuu ya kandanda ya Ujerumani, Bundesliga, msimu wa 55, hawakufaulu kushinda makombe mawili msimu huu na kushindwa kumpa kocha wao Jupp Heynckes zawadi katika mechi yake ya mwisho kama mkufunzi wa klabu hiyo. Heynckes anastaafu na nafasi yake itachukuliwa na kocha wa Frankfurt, Nico Kovac, msimu ujao wa 56 wa Bundesliga.
Mwandishi:Josephat Charo/ap/afpe