FRANKFURT: Mustakbali wa kampuni ya magari ya Opel ni salama
5 Machi 2005Maelfu ya ajira zimeokolewa katika kampuni ya kutengeneza magari ya Kijerumani ya Opel baada ya kampuni hiyo tanzu ya kampuni kubwa kabisa ya kutengeneza magari duniani ya General Motors kupatiwa kondarasi ya kutengeneza magari ya GM ya kiwango cha wastani kwa ajili ya kipindi cha usoni barani Ulaya.
Ushindani wa kuwania kondarasi hiyo mpya ulikuwa kati ya Opel na kampuni nyengine tanzu ya General Motors ya Saab ilioko nchini Sweden.Kampuni hiyo imesema katika taarifa imebaini kwamba kutengeneza magari katika kiwanda cha Rüsselsheim karibu na Frankfurt kutakuwa na ufanisi wa mamilioni ya uero kwa kulinganishwa na kiwanda hicho cha Sweden. Wafanyakazi wa Opel wamekubali kuridhia mambo mengi ili kuweza kuendelea na ajira zao ikiwa ni pamoja kudhibiti mishahara hadi mwaka 2010 na kuwa na masaa zaidi ya kazi yatakayoweza kubadilika kwa kuzingatia hali halisi.
Badala yake menejimenti imeahidi kutotekeleza hatua za kuwaachisha watu kazi au kufunga kiwanda chochote kile hadi mwaka 2010.