Frankfurt. Mgomo wa madereva wa treni waanza leo.
14 Novemba 2007Chama cha waendesha treni nchini Ujerumani GDL kimeitisha mgomo mwingine mkubwa , katika juhudi zake za kusisitiza madai yao ya nyongeza ya asilimia 30 ya mishahara. Mwenyekiti wa GDL Manfred Schell amewaambia waandishi wa habari mjini Frankfurt , kuwa mgomo huo ambao utahusisha matreni ya mizigo utaanza mchana leo Jumatano, wakati mgomo dhidi ya treni za abiria pamoja na treni ziandazo mbali utanza saa 10 baadaye. Mgomo huo utaendelea hadi mapema siku ya Jumamosi. Schell amesema kitakachoendelea baada ya hapo kitakuwa jukumu la viongozi wa reli. GDL kimekuwa kikikataa kurejea katika meza ya majadiliano hadi pale utawala utakapoongeza pendekezo lake la nyongeza ya asilimia 10 ili kuweza kupata muafaka wa kufanyakazi kwa saa nyingi zaidi.