Fischer aonya tena dhidi ya kushirikishwa NATO Iraq.
7 Februari 2004Matangazo
MUNICH: Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Joschka Fischer ameonya tena dhidi ya kupelekwa wanajeshi wa NATO Iraq. Mwanzoni mwa Mkutano wa Kimataifa wa Usalama mjini Munich Bwana Fischer alisema ukweli wake unamlazimisha asifiche kitu juu ya mada hii. Hata hivyo, Ujerumani haitokuwa kizingiti kwa NATO ikiwa umoja huo utaamua kwa jumla kuchukua msimamo mwengine kupita wake. Lakini Ujerumani kabisa haitopeleka wanajeshi wake Iraq, alisema. Wakati huo huo Bwana Fischer alitoa mwito wa kuwa ugaidi uzidi kupigwa vita, na siyo tu kuwa nchi zitie makali siasa zao za ulinzi bali pia kuongeza juhudi za kuzikarabati nchi za Kiarabu, alisema. Mnamo siku mbili zijazo, jumla ya wanasiasa, wanajeshi na mabingwa 280 kutoka nchi 45 watajishughulisha na mustakabali na maendeleo ya Shirika la NATO.