FINALI YA KOMBE LA DUNIA LA KLABU BINGWA MJINI TOKYO INAFUATWA KESHO JUMAPILI NA FINALI YA KOMBE LA KLABU BINGWA AFRIKA MJINI ABUJA,NIGERIA.
10 Desemba 2004Leverkusen iliizaba Dynamo Kiev ya Ukrain mabao 3-0 kutokana na mabao ya kipindcha pili yaliotiwa na Juan, Voronin na Bobic.
Leverkusen,iliohitaji ushindi kuhakikisha inaingia duru ijayo,ilibomoa ngome ya Kiev pale Juan kutoka Brazil,alipoutia kichwa mpira hadi wavuni mwa lango la Kiev mnamo dakika ya 77 ya mchezo.
Kwa ushindi huo,Leverkuesen,iliipiku Real Madrid ya Spain, mabingwa mara 9 wa Kombe hili na kushika uongozi wa kundi lao.Real hatahivyo,pia imo katika duru ijayo ya timu 16 baada ya kuizaba Roma mabao 3-0.
Jogoo la Bayern Munich kutoka Holland,Roy Makaay liliwika tena pale Bayern Munich ilipovunja mwiko kwa wa daima kushindwa katika uwanja wa Ajax Amsterdam.Makaay aliufumania mlango wa Ajax mnamo dakika ya 9 ya mchezo,lakini baadae Tomas Galasek alisawazisha dakika 7 kabla kipindi cha mapumziko.Halafu mnamo dakika ya 64,Ajax ilitangulia kwa bao la pili alilotia Nicolae Mitea .Michael Ballack nae dakika 12 kabla ya firimbi ya mwisho akatia bao la kusawazisha mabao 2:2. Kwa suluhu hiyo timu zote mbili-Ajax na Bayern Munich zinaingia duru ijayo ya kutoana.
Miongoni mwa timu nyengine zilizokata tiketi zao katika duru ijayo ni Chelsea,Manchester United ,Arsenal London na Liverpool-zote za Uingereza.Hapo Uingereza imeipiku Ujerumani kwa kutia timu 4 kwa 3 za Ujerumani.
FINALI YA KOMBE LA KLABU BINGWA AFRIKA:
Mwishoni mwa wiki hii mashabiki wa dimba wanakodoa macho katika finali 2:moja ya klabu bingwa barani Afrika kati ya mabingwa Enyimba na Etoil Sahel mjini Abuja ,Nigeria.Finali ya pili ni ile ya leo juammosi mjini Tokyo,Japan kuania taji la klabu bingwa ya dunia kati ya mabingwa wa Ulaya FC Porto ya Ureno na Once Caldas ya Colombia.
Ama mabingwa wa zamani wa Kombe la Amerika Kusini:Olympia,mambo yamewaendea msimu huu kombo:
Miaka 2 nyuma Olympia waliibuka mabingwa wa dunia wa klabu bingwa baada ya kuiporomoa Real Madrid ya Spain mjini Tokyo,kutwa taji hilo mjini Tokyo.
Jumapili iliopita Olimpia ilizabwa mabao 3-1 na Guarani mbele ya mashabiki 530 tu uwanjani na hivyo imekwama mkiani mwa Ligi ya Paraguay.
Kwa kweli,Olimpia ni klabu maarufu katika dimba la Amerika Kusini,lakini tangu kuondokewa na rais wao Oswaldo Dibb mambo hayawaendei uzuri.Chini ya uongozi wake olimpia,ilishinda Kombe la klabu bingwa la Amerika Kusini-Libertadores Cup tena mara 3,1979,1990 na 2002.Rekodi hiyo ya Olimpiya haikufikiwa hata na klabu za Brazil isipokuwa imepindukiwa na Independiente na Boca Juniors za Argentina.Lakini pia Penarol na Nacional za Uruguay.
FINALI YA KOMBE LA AFRIKA LA KLABU BINGWA:
Kesho ni finali ya Kombe la klabu bingwa barani Afrika –Enyimba mabingwa watetezi wanakutana kwa changamoto ya mwisho ya kuamua hatima ya kombe hili mwaka huu na mahasimu wao Etoile du Sahel ya Tunisia.Duru ya kwanza ya finali hii ilimalizika 2:1 .
Mjini Abuja,wachezaji wa klabu bingwa ya Afrika-Enyimba wameahidiwa ardhi iwapo watafuta mabao 2:1 waliochapwa na Etoil du sahel, jumamosi iliopita mjini Sousse,Tunisia na kulibakisha kombe hilo nyumbani Nigeria.
Msemaji wa Enyimba Tonnex Chukwu amehakikisha kuwa diwani wa jiji la Abuja,Nasir El-Rufai amewaahidi viwanja mjini Abuja, wachezaji na wakuu wa klabu ya Enyimba.
Enyimba ni klabu ya kwanza ya Nigeria kutwaa Kombe la klabu bingwa barani Afrika mwaka jana na kesho basi inataka kuigiza T.P Mazembe ya Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo,klabu pekee ya Afrika iliothubutu kuiltwaa Kombe hilo mara 2, 1967 na 1968.
Katika duru ya kwanza ya finali hii mjini sousse,Tunisia, ilikua Enyimba iliotangulia kutia bao, kila timu ilicheza na wachezaji 10.Mmmoja alitolewa nje na rifu kila upande.
KOMBE LA SHIRIKISO LA AFRIKA:
Kura ilipigwa juzi alhamisi mjini Cairo kuamua duru ya kwanza,yapili na ya tatu ya Kombe la shirikisho la dimba la Afrika. Klabu 48 zimejiandikisha kuania Kombe hilo.
Miongoni mwa timu hizo ni Kipanga ya Zanzibar,ambayo klabu zake zinashiriki kwa mara ya kwanza msimu ujao katika vikombe vya CAF-shirikisho la kabumbu la Afrika.N yengine ni Prision kutoka Tanzania bara,Kampala City Council ya Uganda Chemelil Sugar ya Kenya.APR itaiwakilisha Rwanda.
Miongoni mwa klabu nyengine ni Unuion Douala ya Kameroun,Arab Contractors ya Misri,SuperSport united ya Afrika Kusini na Muni Sport ya Congo.
MABONDIA:
Usiku wa leo,itakua asie na mwana aeleke jiwe na asie na mguu atie gongo-mkutano ringini huko Las Vegas,Marekani:Danny Williams aliemchezesha klindumbwendumbwe Mike Tyson ,anajitosa ringini kupambana na Muukraine mwenye kambi yake Ujerumani, Vitali Klitischko.Williams anadai kwamba, klitschko hana ari ya kupigana kwa kadiri ya kuweza kulitetea taji lake la WBC la wezani wa juu ulimwenguni.Danny Williams anajaribu kuthibitisha nguvu zake zilizomuwezesha kumtwanga Mike Tyson miezi 5 iliopita.Williams amemudu kumaliza duru 12 za ndondi mara 5 katika changamoto zake 35 wakati klitschko amefika umbali huo mara moja tu.