1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

FIFA yawaadhibu maafisa wake

18 Novemba 2010

Shirikisho la kandanda duniani FIFA limetangaza kuwasimamisha wajumbe wawili wa kamati yake ya utendaji, kutokana na kashfa ya kutaka rushwa.

https://p.dw.com/p/QCbP
Picha: DW

Wajumbe hao Amos Adamu kutoka Nigeria na Reynald Temarii wa Ocenia, wanatuhumiwa kuomba rushwa ili kutoa upendeleo wakati wa upigaji kura kuchagua wenyeji wa fainali za dunia za mwaka 2018 na 2022.

Kamati ya maadili ya FIFA baada ya kufanya uchunguzi imeamua kuwasimamisha wajumbe hao ambapo Amos Adamu amesimamishwa kwa muda wa miaka mitatu kutoka katika kamati hiyo na kutojihusisha na masuala yoyote ya soka.Reynald yeye amepewa adhabu ya kusimamishwa kwa muda wa mwaka mmoja.

Mbali ya kifungo hicho, pia wajumbe hao wamepigwa fainali, ambapo Adamu ametozwa faini ya dola 10,000 wakati Reynald ametozwa faini ya dola 5,000.

Wajumbe hao wa kamati ya utendaji sasa kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa FIFA Jerome Valcke, hawatoshiriki katika upigaji kura kuchagua wenyeji wa fainali hizo, kura ambazo zitafanyika tarehe 2  Disemba

Nchi zinazowania uenyeji wa fainali za mwaka 2018 ni pamoja na Uingereza, Urusi, ushirikiano wa Ureno na Uhispania na ushirikiano wa Uholanzi na Ubelgiji.Marekani, Australia, Japan, Qatar na Korea Kusini zinawania kuandaa fainali za mwaka 2022.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/AFP