Utoaji kibali cha Kombe la Dunia 2026 wacheleweshwa
10 Juni 2015Badala yake, shirikisho hilo limeanza shughuli ya kumtafuta mrithi wa rais wake anayeondoka, Sepp Blatter.
Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome Valcke, amesema kuwa litakuwa "jambo lisilo maana" kuanza mchakato wa kutoa kibali hicho kwa wakati huu. Wakati huo huo, FIFA imesema kuwa kamati yake kuu itaandaa mkutano maalum mwezi Julai ili kujadili kuhusu "mapendekezo kadhaa" ya tarehe za kuandaliwa mkutano wa baraza kuu utakaomchagua atakayechukua nafasi ya Blatter.
Kura ya kuitafuta nchi itakayoandaa kombe la dunia mwaka 2026 inatarajiwa kufanyika mjini Kuala Lumpur mwezi Mei mwaka 2017.
Marekani iko kifua mbele kuandaa michuano hiyo lakini Canada, Mexico na Colombia pia zimewasilisha maombi ya kutaka kuwa wenyeji wa tamasha hilo
Urusi na Qatar zilichaguliwa kuandaa michuano ya mwaka 2018 na 2022 kupitia kura ya siri iliopigwa na wanachama wakuu wa FIFA wapatao 22 mnamo mwezi Disemba mwaka 2010. Lakini viongozi wa mashtaka nchini Uswizi wanachunguza madai ya ufisadi yanayozunguka zabuni hizo.
Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef