1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

FIFA tayari kushughulikia malalamiko ya kupunguzwa mishahara

6 Aprili 2020

Shirikisho la Kandanda Duniani – FIFA liko tayari kuyashughulikia malalamiko na rufaa kuhusiana na kuwapunguzia wachezaji mishahara kutokana na janga la virusi vya corona

https://p.dw.com/p/3aXqr
Symbolbild FIFA
Picha: picture-alliance/dpa/KEYSTONE/E. Leanza

Tukibaki na suala hilo la vilabu na mishahara, ni kuwa Shirikisho la Kandanda Duniani – FIFA liko tayari kuyashughulikia malalamiko na rufaa kuhusiana na kuwapunguzia wachezaji mishahara, kutoa miongozo kwa vilabu na mashirika ya kandanda yanayotaka kupunguza gharama kipindi hiki ambacho michezo imesitishwa kutokana na janga la virusi vya corona. Hayo ni kwa mujibu wa nakala ya ndani ya FIFA iliyoonyeshwa kwa shirika la habari la Reuters.

Suala la kupunguzwa mishahara ya wachezaji limeripuka, wakati utata au ubishani ukizuka nchini England huku nchi nyingine kama vile Ujerumani na Uhispania, wachezaji wamekubali kupunguziwa kwa muda mishahara yao.

Jopokazi la FIFA kuhusu janga la virusi vya corona lilikutana wiki iliyopita na kukubuliana kuhusu msururu wa masuala yaliyoorodheshwa kwenye nakala hiyo, ikiwa ni pamoja na kuwa mikataba ya wachezaji iliyopaswa kukamilika Juni mwaka huu inapaswa kurefushwa hadi mwisho mwa msimu wowote ulioendelezwa.