FIFA kuchapisha ripoti kamili kuhusu ufisadi
19 Desemba 2014Akizungumza katika mkutano wa siku mbili wa kamati kuu ya FIFA, ulioandaliwa mjini Marrakech, Morocco, Rais wa FIFA Sepp Blatter amesema ripoti hiyo itachapishwa “katika mfumo sahihi” baada ya uchunguzi kuendelea kufanywa dhidi ya maafisa kadhaa wakuu wa FIFA kuhusiana na michakato ya kutafuta vibali vya kuandaa fainali za Kombe la Dunia 2018 na 2022. Hata hivyo Blatter amesema ripoti hiyo “inahusu historia” kumaanisha kuwa yaliyopita, na akasema anataka kuangazia siku za usoni.
FIFA imechukua hatua hiyo kufuatia wito wa kuitaka ichapishe kikamilifu ripoti ya mchunguzi wa kamati ya maadili Michael Garcia kuhusiana na upelelezi wa kutolewa vibali vya kuandaa Kombe la Dunia Urusi 2018 na Qatar 2022. Garcia, mwanasheria wa zamani wa Marekani alijiuzulu Jumatano kutoka kamati ya maadili ya FIFA, akisema amepoteza imani na Hans-Joachim Eckert, mwenyekiti wa jopo la uchunguzi la kamati hiyo ya maadili.
Uamuzi huo unafuatia hatua ya FIFA kulipuuzilia mbali ombi la Garcia kupinga tathmini iliyofanywa na Eckert kuhusiana na ripoti yake hiyo, akisema kuwa ripoti hiyo haikutoa picha halisi ya mambo aliyoyagundua katika uchunguzi wake. Kamati kuu imekubaliana kumteua wakili Mswisi Cornel Borbely kama kaimu mwenyekiti wa jopo la upelelezi la kamati huru ya maadili kuchukua nafasi ya Garcia.
Mwandishi. Bruce Amani/AFP/reuters
Mhariri: Yusuf Saumu