Fidel Castro aaga dunia akiwa na miaka 90
26 Novemba 2016HAVANA:
Kiongozi mashuhuri ,mwanamapinduzi , aliekuwa Rais wa Cuba,Fidel Castro amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 90.Taarifa juu ya kifo cha mwanamapinduzi huyo ilitolewa, na ndugu yake, Rais Raul Castro kwenye televisheni ya serikali alisema: " Wapendwa watu wa Cuba, marafiki wa Amerika yetu na dunia nzima, nikiwa na majonzi mazito, nawapa taarifa ,kwamba kamanda mkuu wa mapinduzi ya Cuba,Fidel Castro Ruz amefariki dunia."
Fidel Castro aliiongoza Cuba, baada ya kuyafanikisha mapinduzi yaliyoung'oa utawala wa dikteta Fulgencio Batista mnamo mwaka wa 1959. Hatua alizochukua ikiwa pamoja na kuleta mageuzi katika sera ya ardhi na kutaifisha viwanda na makampuni , zilisababisha uadui kati yake na Marekani.
Marekani ilijibu kwa kuiwekea Cuba vikwazo vya kibiashara. Hata hivyo Cuba ilipata misaada mikubwa kutoka Umoja wa kisoviet na hivyo kuwa tegemezi wakati wote. Kisiwa cha Cuba kiliingia katika kipindi kigumu sana cha matatizo ya kiuchumi baada ya Umoja wa kisoviet kusambaratika mnamo mwaka wa 1990 .Hata hivyo mfumo wake wa kikomunisti uliweza kukihimili kipindi hicho hadi hivi karibuni ambapo Cuba na Marekani zilirejesha uhusiano wa kibalozi baina yao.
Rais wa Venezuela Nicholas Maduro amemsifu Fidel Castro kwa uongozi wake. Nae kiongozi wa zamani wa urusi Mikhael Gorbachev amemsifu Castro kwa kuiimarisha Cuba.
Mwandishi: Zainab Aziz/afpe, ape
Mhariri: Daniel Gakuba