1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Felix Tshisekedi kuwania muhula mwingine wa rais mwaka 2023

Saleh Mwanamilongo
13 Mei 2021

Akiwa ziarani mjini Lubumbashi, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi ametangaza nia yake ya kuwania muhula wa pili ifikapo mwaka 2023.

https://p.dw.com/p/3tLCO
DR Kongo  Kinshasa Vereidigung Präsident Felix Tshisekedi
Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Delay

Hiyo ni ziara ya kwanza ya rais Felix Tshisekedi jimboni Katanga,toka kuvunjika kwa muungano wake wa kiasa na Joseph Kabila. Akiwahutubia hadharani wakaazi wa mji huo, Tshisekedi ameweka wazi niya yake ya kuwania muhula mwingine wa rais.

'' Nitawaletea mradi mpya utakaochangia maendeleo ya Congo. Mtaona jinsi tutakavyo badili hii Congo hadi tufikie uchaguzi wa mwaka 2023. Nitarejea tena hapa  kwenu ilikuwaomba mnipigie kura kwenye uchaguzi wa mwaka 2023'', alisema Tshisekedi.

 Rais Tshisekedi amewaomba raia wa jimbo hilo la Katanga kuunga mkono juhudi zake za kuleta amani huko Kivu ya kaskazini na Ituri. Huku akiwakosoa vikali wapinzani wake. Tshisekedi amesema wale wote wanaopinga hatua yake ya kutangaza hali ya dharura huko mashariki mwa Congo kuwa ni wachawi na wasioipenda Congo.

''Propaganda za uongo kwa raia''

Karikatur von Meddy | DR Kongo

Upinzani umelaumu matamshi hayo ya rais Tshisekedi na kusema amekuwa akiongoza nchi kwa vitisho. Ferdinand Kambere ni naibu katibu mtendaji wa chama cha PPRD cha, rais wa zamani Joseph Kabila.

''Ukiwa mpizani wake (Tshisekedi) kimawazo au kimafikara mara moja umekuwa mchawi  na mtu mbaya. Sifahamu nchi yetu inaelekea wapi. Demokrasia tuliotegemea leo imekuwa ni ndoto tu'',alisema Kambere.

 Ferdinand Kambere amesema rais Tshisekedi hana niya ya kuitisha uchaguzi ifikapo mwaka 2023, kwa sababu hakuna ishara yoyote ya mageuzi ya sheria ya uchaguzi.

''Tumeshuhudia uzembe mkubwa bungeni kuhusu mchakato wa mageuzi ya sheria ya uchaguzi. Hatua yake ya kutangaza kuwa mgombea ni propaganda za uongo kwa raia kwa sababu hana niya ya kwenda kwenye uchaguzi, na raia hawatokubali kutokuwepo na uchaguzi mwaka 2023'',aliendelea kusema Kambere.

Bunge lilitakiwa kupitisha sheria mpya wa uchaguzi toka septemba mwaka jana,lakini kufuatia tofauti za kisiasa mchakato huo uliarishwa.