1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Fedha na mali zingine za Mubarak kuzuiwa?

Abdu Said Mtullya15 Februari 2011

Watu wa Misri wataka Mali za viongozi wa zamani zirejeshwe nchini

https://p.dw.com/p/10HEX
Aliekuwa Rais ya Misri Hosni MubarakPicha: AP

Misri imetoa ombi kwa Marekani, Uingereza na Ufaransa la kuzizuia akiba za benki za waliokuwa viongozi wa ngazi za juu katika utawala wa Rais Hosni Mubarak.

Lakini msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Ufaransa Bernard Valero ameeleza kuwa Misri imeiomba nchi yake izuie akiba za benki za viongozi wengine na siyo za Mubarak na za familia yake.Hata hivyo Uswisi imetangaza kuwa tayari imeshazizuia akiba za Mubarak.

Nchi kadhaa za Ulaya ikiwa pamoja na Ujerumani zimesema kuwa zimelipokea ombi hilo la Misri.Mawaziri wa fedha wa Ulaya leo watakutana mjini Brussels kuzungumzia juu ya Misri ambapo watalijadili ombi la nchi hiyo juu ya kuzizuia mali za Mubarak na za watu wake.

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza William Hague amesema kuwa nchi yake italizingatia ombi la Misri na kwamba itachukua hatua madhubuti na za haraka endapo utapatikana ushahidi juu ya kuibiwa fedha za serikali ya Misri.Akizungumza bungeni waziri Hague alisema kuwa serikali ya Uingereza imepokea ombi la serikali ya Misri la kuzikamata mali za viongozi wa kadhaa waliokuwamo katika utawala wa Rais Mubarak. Waziri Hague aliliarifu bunge kuwa Uingereza imeshachukua hatua kama hiyo kuhusiana naTunisia baada ya rais wa nchi hiyo kuangushwa na watu wake.

Nchini Ujerumani, wizara ya mambo ya nje pia imethibitisha kuwa imelipokea ombi hilo.