1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

FC Cologne-mabingwa wa kwanza wa Bundesliga 1963

Ramadhan Ali29 Mei 2007

FC cologne ambayo sasa inacheza daraja ya pili ya Bundesliga kwa kweli ikitamba miaka ya 1960 kama vile inavyotamba wakati huu Bayern munich.

https://p.dw.com/p/CHc8

Msimu wa Bundesliga-ligi ya Ujerumani ulimalizika wiki 2 zilizopita na jumamosi iliopita, FC Nüremberg,mojawapo wa mabingwa wa zamani wa Ujerumani,waliwapiga kumbo VFB Stuttgart mabingwa wapya msimu huu na kuwazuwia kutoroka na mataji yote 2 ya ubingwa:Kombe la Ligi na la shirikisho la dimba la Ujerumani (DFB-Pokale).Nüremberg,iliizaba Stuttgart mabao 3:2.

“Nadhani umaarufu wa FC Cologne ulikuwa sawa na wa Bayern Munich ulivyo hii leo.”

Hivyo ndivyo anavyokumbuka stadi wa zamani wa FC cologne ,bingwa wa dunia na Ujerumani 1974 na rais wa sasa wa klabu hii Wolfgang Overath.

Overath anajiramba vidole kwa utamu akikumbuka enzi za klabu yake ilivyokuwa ikitamba miaka ya mwanzo ya 1960.Kwani, 1962 -FC Cologne ndio waliibuka mabingwa wa Ujerumani wakifuta enzi za mabingwa mara 9 FC Nüremberg.Mwaka uliofuatia wakaibuka mabingwa wa kwanza kabisa wa Bundesliga-Ligi ya sasa ya Ujerumani ilioasisiwa mwaka huo wa 1963.

Overath anakumbusha:

“Tulikuwa na klabu yetu wenyewe-Geissbockheim wakati timu nyengine zikipiga maskani yao kwenye magereji ya kuegesha magari.Tukivaa jazi nyeupe sawa na Real Madrid na hakuna timu nyengine iliovaa jazi hizo.Katika Bundesliga tulikua usoni kabisa,lakini mwishoe, hatukuitumia barabara nafasi hii ya uongozi.”

Asema rais wa sasa wa FC Cologne ambayo baada ya miaka 50 katika bundesliga,iliteremshwa mara 3 katika daraja ya pili ilioko sasa.Msimu huu imemaliza 9 kati ya timu 18 na sasa inajenga upya kurejea kule inakodai ni nyumbani mwake-daraja ya kwanza.

Rais wa enzi zile ilipokua Cologne ikitamba Franz Kremer ni miongoni mwa waasisi walioanzisha bundesliga.Ni wazi kwamba klabu yake hii ilinufaika tangu kutokana na mawazo yake hata umaarufu wake.Kwanza aliwachagua wachezaji-chipukizi kutoka mitaa ya karibu na Cologne akina Wolfgang Weber na wolfgang Overath.

Na rais wa sasa Overath anakumbuka:

“Ilikuwa mjini Saarbrücken, ambako tulishinda kwa mabao 2:0 na nilitia bao la kwanza.Lilitokana na pasi mbili za kurejesheana kati yangu na Hans Schafer.Na huo ukawa mwanzo wa kutawazwa mabingwa wa Ujerumani.”

Katika miaka iliofuatia ,FC Cologne ikicheza kati ya timu kali za usoni kabisa,lakini kuvaa taji la 3 ilibidi kusubiri hadi msimu wa 1968.1968 ikatwaa kombe lake la kwanza kabisa la shirikisho la dimba la Ujerumani-DFB Pokale kama ilivyofanya juzi Nuremberg.Kocha Hennes Weisweiler,ni mmoja kati ya makocha wachawi nchini Ujerumani zama zake akachukua dhamana ya timu hii 1976 na hakukawia kuwika kama jogoo:Kwani alitwaa mara mbili kombe la shirikisho la Ujerumani.Vikombe hivyo 2 vikawa zawadi ya uchungu mkubwa kwa rais wa sasa Wolfgang Overath.Kwani, baada ya mvutano mkubwa usiokwisha na kocha Weisweiler,aliamua Overath kustaafu kucheza dimba.Bila ya Overath timu ya chipukizi wapya ya FC cologne iliendelea kutamba na 1978 ikatawazwsa mabingwa bundesliga na wa kombe la shirikisho la dimba la Ujerumani kwa mpigo mmoja.Taji lake la mwisho kabisa FC Cologne ililivaa 1983 ilipoilaza Fortuna Düsseldorf,hasimu yake mkubwa katika mto Rhein wakati ule kwa bao 1:0 .Kuanzia hapo Fc Cologne ikaanza kuteremka chini .

Yakaanza mabishano kati ya wachezaji wake mashuhuri na maarufu kabisa alikuwa kipa wa taifa Toni Schumacher.1987 akaiachamkono klabu yake maarufu kwa kuwa katika kitabu chake alichokiita “Anpfiff”-firimbi imelia –aliwakashifu wachezaji wenzake.Alipasua kuwa wengine wakitumia madawa ya kulevya na wengine wakienda madanguroni.Miaka 8 baadae,FC Cologne iliposadifu kuadhimisha mwaka wa 50 tangu kuasisiwa, ikateremshwa daraja ya pili.Tangu 1998 FC Cologne imeteremka daraja ya pili mara 4-ikipanda na kuteremshwa.Hii lakini haikuwavunja mashabiki wake kusheheni uwanjani hadi 40.000 wanapocheza-ni rekodi kwa timu ya daraja ya pili barani ulaya.

Kocha wao mpya ambae alitarajiwa msimu wa 2005 awapandishe juu tena Uwe Rapöolder,alitimuliwa baada ya kupita nusu mwaka tu.Aliona mambo ni moto mjini Cologne.

Viongozi wa klabu hii maarufu iliopatwa sasa na mkosi wafanye nini sasa ili kuirejesha FC Cologne jina lake la zamani ?

Rais wake wa sasa Wolfgang Overath anasema:

“jibu ni gumu laiti mtu angelijua.Kimsingi,naamini kuna daima kupanda na kushuka na mtindo huu kitambo sasa ukiendelea.”

Wakati umewadia kuelekea daraja jnyengine-akikusudia hapo FC Cologne ambayo mascoat wake ni beberu ,chini ya kocha wake maarufu Christopher daum irudi daraja ya kwanza mwishoni mwa msimu ujao:

Kwani Geisbock-beberu wa FC cologne amechoka kunguruma daraja ya kwanza: