FBI yaanzisha uchunguzi mpya dhidi ya Clinton
2 Novemba 2016Matokeo ya uchunguzi huo na wakati yatakapotolewa haijulikani lakini athari za uchunguzi huo wa shirika hilo la FBI tayari zimeanza kuonekana katika ushindani huo mkubwa wa ikulu ya Marekani.
Matokeo ya hivi punde zaidi yalionyesha kuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Republican Donald Trump yuko mbele ya Clinton kwa mara ya kwanza tangu mwezi Mei.
Matokeo hayo ya mwezi Oktoba yamewashangaza wengi na kumueka Clinton katika nafasi ngumu huku wafuasi wa chama cha Democrat wakimkosoa mkuu wa shirika hilo la FBI James Comey kwa kukiuka kanuni na utaratibu kwa kuanzisha upya uchunguzi dhidi ya Clinton kuhusiana na jinsi alivyoshughulikia barua pepe za serikali karibu na uchaguzi mkuu.
Robby Mook, meneja wa kampeini za Clinton alilalamika kwa kusema kuwa mkuu huyo wa FBI amekuwa akisema kuwa kuna habari mpya. Aliongeza kuwa, " tulitambua kuwa hana hata ruhusa ya kujuwa kilichomo".
Hata hivyo Trump hakutaja lolote kuhusiana na matokeo hayo lakini mgombea mwenza wake wa wadhifa wa makamu wa rais Mike Pence alifichuwa katika ripoti hiyo kuwa , ushindi uko upande wao. Alisema kuwa ripoti ya hivi punde inaonyesha kuwa Donald Trump anaongoza kote nchini humo. Pence alisema, "sasa vuguvugu linaunganika, Pennsylvania inakuja pamoja , na sote kwa pamoja tutamwezesha Donald Trump kuwa rais mpya wa Marekani."
Siku ya Ijumaa Comey aliliambia bunge kuwa shirika hilo limetambua kuweko kwa barua pepe hizo. Alisema kuwa zinapaswa kuangaziwa tena kwasababu huenda zikawa muhimu katika uchunguzi wa awali dhidi ya Clinton katika matumizi ya barua hizo pepe. Ni hatua ambayo imepokelewa kwa hisia mbali mbali na wananchi nchini humo.
Maoni ya wapiga kura kuhusiana na uchunguzi huo
David Stenger mpiga kura nchini humo alisema kuwa hali ya kwamba FBI imeanzisha upya uchunguzi huo, inaonyesha kuwa Clinton alifanya mamabo mengi zaidi ambayo bado hawafahamu.
Lakini pia kuna wale wenye maoni tofauti na hayo kama anavyosema Kim Chappell kwamba katika uchunguzi wa awali kuhusiana na kisa hicho cha barua pepe hakuna lolote la maana lililofichuliwa hivyo basi haoni kuwa kutakuwa na lolote jipya.
Clinton pia alichunguzwa kwa kutoa msamaha kwa Marc Rich mumewe mmoja wa wafadhili wa kampeini yake. Rich alikuwa anaishi ng'ambo wakati huo kuepukana na mashtaka yanayohusiana na ukiukaji wa kikwazo kilichokuwa kimewekwa kwa kusafirisha bidhaa nchini Iran. Alifariki mwaka 2013.
Ni mikimbio ya mwisho mwisho hii katika kinyang'anyiro cha urais nchini Marekani ambapo kilele cha yote kitakuwa tarehe 8 mwezi huu wakati raia wa nchi hiyo watakapokata kauli kuhusu yule watakayemchagua kuwaongoza kama rais na amiri mkuu wa majeshi nchini humo.
Mwandishi. Tatu Karema/ DPA/ AFPE
Mhariri:Iddi Ssessanga