1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Faye aahidi kuitawala Senegal kwa unyenyekevu

26 Machi 2024

Mgombea wa upinzani Senegal Bassirou Diomaye Faye anajiandaa kuwa rais baada ya mpinzani wake mkuu kutoka chama tawala kukubali kushindwa, kufuatia uchaguzi uliofanyika siku chache tu baada ya Faye kuachiliwa huru.

https://p.dw.com/p/4e750
Raia mteule wa Senegal Bassirou Diomaye Faye
Rais mteule Bassirou Diomaye Faye mwenye umri wa miaka 44, ameapa kutawala kwa unyenyekevu na uwazi Picha: Luc Gnago/REUTERS

Miezi michache tu iliyopita, mtu anayetarajiwa kuwa rais ajaye wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye, alikuwa amekaa kwenye chumba cha gezera. Mtu ambaye hakufahamika sana nje ya chama chake cha upinzani cha Pastef.

Kila kitu kilibadilika wakati kiongozi wa chama chake, mwenye umaarufu mkubwa, Ousmane Sonko, ambaye alikuwa pia kizuizini, alishitakiwa kwa uasi mwezi Julai na kuzuiwa kugombea katika uchaguzi ili kumrithi Rais Macky Sall.

Hiyo ilisafisha njia kwa Faye kuibuka kutoka kivuli cha bosi wake wa zamani na hatimaye kutoka gerezani, kuchukua kijiti na jana Jumatatu, - siku yake ya kutimiza miaka 44 ya kuzaliwa – kuibuka mshindi baada ya mpinzani wake kukiri kushindwa.

Mpinzani ashinda uchaguzi kwa mara ya kwanza

Waziri mkuu wa zamani Amadou Ba akiri kushindwa
Amadou Ba wa muungano tawala wa Benno Bokk Yakaar alikiri kushindwa katika uchaguzi wa raisPicha: Luc Gnago/REUTERS

Ni mara ya kwanza katika chaguzi 12 za urais zilizofanyika chini ya haki ya upigaji kura wa watu wote tangu Senegal ilipopata uhuru kutoka kwa Ufaransa mwaka wa 1960 ambapo mgombea wa upinzani ameshinda katika duru ya kwanza ya upigaji kura.

Mpinzani wake mkuu kutoka muungano unaotawala, Amadou Ba, mwenye umri wa miaka 62, ameutambua ushindi wa Faye na kumpigia simu kumpa salamu za pongezi.

Rais anayeondoka Macky Sall, ambaye hakugombea baada ya ushindi wake wa 2012 na 2019, pia amempongeza, akisifia kile alichokielezea kuwa ni "ushindi wa demokrasia ya Senegal." Katika hotuba yake ya kwanza baada ya uchaguzi, Faye amewaambia waandishi habari kuwa katika kumchagua yeye, watu wa Senegal wameamua kuwachana na yaliyopita. Ameahidi kutawala kwa unyenyekevu na uwazi.

Aidha, amemshukuru Rais Macky Sall na wagombea wengine kwa kuheshimu utamaduni wa demokrasia wa Senegal kwa kutambua ushindi wake mapema kabisa kabla ya matokeo rasmi kutolewa. Hatua ya Ousmane Sonko kumuidhinisha naibu wake huyo wa zamanikabla ya uchaguzi wa Jumapili ilikuwa muhimu.

"Sonko mooy Diomaye, Diomaye mooy Sonko,”

Faye na Sonko wakitangaza ushirikiano wao
Kiongozi wa upinzani Ousmane Sonko (Kulia) akimuidhinisha aliyekuwa naibu wake Bassirou Faye kugombea uraisPicha: John Wessels/AFP/Getty Images

"Chaguo langu la Diomaye sio chaguo kutoka moyoni, bali la hoja. Nilimchagua kwa sababu anatimiza vigezo ambavyo nimeviweka. Ni mchapakazi na amesoma katika shule ya kifahari kabisa nchini Senegal,” Alisema Sonko kwenye ujumbe wa video

"Hakuna anayeweza kusema sio mwaminifu. Naweza hata kusema kuwa ni mwaminifu zaidi kuniliko. Ninamkabidhi mradi huu mikononi mwake,” Alisema Sonko akiongeza kuwa "Bassirou ni mimi.”

Baada ya kuwachiwa kutoka gerezani Machi 14, washirika hao walianza mfululizo wa kampeni na kupokelewa na umati wafuasi waliokuwa na furaha, walioimba "Sonko mooy Diomaye, Diomaye mooy Sonko,” au "Sonko ni Diomaye, Diomaye ni Sonko.”

Mkaguzi huyo wa zamani wa ushuru, aliyejinadi kama sehemu ya kizazi kipya cha wanasiasa, anaamini katika uhuru wa kitaifa, ugavi wa haki wa mali, na mageuzi ya kile anachokiona kama mfumo wa haki mbovu.

Wafuasi wa Faye na Sonko
Faye aliyejinadi kuwa sehemu ya kizazi kipya cha wanasiasa alipata umaarufu mkubwa miongoni mwa vijana Picha: Muhamadou Bittaye/AFP/Getty Images

Matokeo rasmi kutangazwa mwishoni mwa wiki

Tume ya uchaguzi imesema matokeo ya awali yalionyesha Faye akiwa na karibu asilimia 53.7 ya kura na Amadou Ba akiwa na asilimia 36.2 kwa kuzingatia hesabu kutoka asilimia 90 ya vituo vya kupigia kura katika duru ya kwanza ya uchaguzi. Matokeo rasmi yanatarajiwa kutangaza ifikapo mwishoni mwa wiki hii.

Kurasa za mbele za magazeti tayari zimempongeza Faye. "Heri ya Siku ya Kuzaliwa Mheshimiwa Rais,” liliandika gazeti la Walf Quotidien, likirejelea Jumatatu kuwa siku ya kuzaliwa Faye. Karibu watu milioni 7.3 kati ya idadi ya watu milioni 18 nchini Senegal walikuwa na haki ya kupiga kura. Uchaguzi huo ulifuatiliwa kwa karibu ikizingatiwa kuwa Senegal inatazamwa kuwa mwanga wa demokrasia katika eneo la Afrika Magharibi. Mamia ya waangalizi wa uchaguzi wakiwemo wa mashirika ya kiraia, Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Maendeleo ya Afrika Magharibi – ECOWAS na Umoja wa Ulaya walisema zoezi hilo lilifanyika kwa utulivu, ufanisi na kwa njia nzuri.

AFP, AP, Reuters, DPA