1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano mkuu wa Fatah.

Abdu Said Mtullya4 Agosti 2009

Mkutano mkuu wa chama cha Fatah unaendelea mjini Bethlehem .

https://p.dw.com/p/J3au
Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas.Picha: AP


Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas amekitaka chama chake cha Fatah kijijenge upya ili kiweze kukabiliana na changa moto zilizopo.

Bwana Mahmoud Abbas ametoa mwito huo kwenye mkutano mkuu wa chama chake unaofanyika mjini Bethlehem kwa mara ya kwanza baada ya miaka 20.

Akiwahutubia wajumbe katika ufunguzi wa mkutano huo kiongozi huyo wa wapalestina pia alikiri makosa mengi yaliyofanywa na chama cha Fatah.

Lakini amepinga madai kwamba mapambano halali yanayoendeshwa na chama chake kuwa ni ugaidi.Amesema wapalestina wana haki ya kuendesha mapambano hayo ili kupinga kukaliwa kwa ardhi yao.

Bwana Mahmoud Abbas amekumbusha kuwa chama cha Fatah kilipinga ugaidi wakati kiongozi wake wa hapo awali Yassir Arafat alipotangaza uhuru wa Palestina mnamo mwaka 1988.Abbas amesema huo ndio utakuwa msimamo thabiti wa Fatah.

Bwana Abbas pia amewataka wapalestina wajizatiti katika kuendelea na mazungumzo ya kuleta amani katika mashariki ya kati. Ameeleza kuwa wapalestina wanaopigania nchi yao wanataka amani lakini wana haki ya kuendeleza mapambano halali.

Akisisitiza juu ya umuhhimu wa mkutano huo mjumbe wa kamati kuu ya chama cha Fatah Nabil Shahal amesema suala lililopo ni kutumia fursa ya mkutano huo ili kusonga mbele.

Hatahivyo katika hotuba yake rais wa mamlaka ya Palestina bwana pia alizungumzia juu ya makosa yaliyofanywa na chama chake cha Fatah. Amekiri kwamba makosa hayo ndiyo yaliyosababisha chama cha Fatah kishindwe katika uchaguzi mkuu uliofanyika miaka mitatu iliyopita na kutimuliwa kutoka Ukanda wa Gaza.

Ameyataja makosa hayo kuwa pamoja na kukwama kwa mchakato wa amani, na tabia za chama zinazopingwa na wananchi, udhaifu katika utekelezaji, ,kufarakana na wananchi na utovu wa nidhamu.

Chama cha Fatah kilikuwa kinawaongoza wapalestina wote hadi kiliposhindwa vibaya na mahasimu wao wa Hamas katika uchaguzi wa mwaka 2006.Chama cha Fatah kinalaumiwa kwa mkakati wake wa kutelekeza mapambano ya mtutu wa bunduki na pia kinalaumiwa kwa kuweka kando ahadi yake ya kuitokomeza Israel.Sambamba na hayo chama hicho kimekuwa kinapoteza imani kutokana na kushindwa kwa juhudi za kuleta amani.

Mkutano mkuu wa siku tatu wa chama cha Fatah unaofanyika katika mji wa Bethlehem kwenye Ukingo wa Magharibi unatarajiwa kupitisha mwongozo mpya wa siasa .

Wajumbe alfu 2200 wanaohudhuria mkutano huo pia watawachagua viongozi wapya.

Mkutano mkuu huo ni wa sita tokea chama cha Fatah kianzishwe mwishoni mwa miaka ya 1950.

Mwandishi/Mtullya.

Mhariri/..