Fatah na Hamas zatia saini makubaliano kuunda serikali ya umoja wa taifa
24 Machi 2008Hati iliyotiwa saini siku ya Jumapili kati ya wawakilishi wa makundi ya Fatah na Hamas,inatoa wito wa kuundwa serikali ya umoja wa taifa na kujengwa upya vikosi vya usalama vitakavyokuwa tiifu kwa serikali ya umoja badala ya makundi mbali mbali.Mjumbe wa Hamas Mussa Abou Marzouk alietia saini hati hiyo mjini Sanaa pamoja na afisa wa Fatah,Azzam al-Ahmed amesema,Azimio la Sanaa ni mwanzo mpya.Rais Abdullah Saleh wa Yemeni akaeleza kuwa majadiliano zaidi kati ya makundi hayo mawili ya Wapalestina yatafanywa tena mnamo mwezi wa Aprili.
Lakini tofauti za maoni zilichomoka saa chache baada ya hati hiyo kutiwa saini.Ofisi ya Rais Abbas imesema,Hamas lazima iache kudhibiti Ukanda wa Gaza kabla ya majadiliano yo yote kuweza kufanywa,kwani hati hiyo inatoa wito wa kurejeshwa hali ya awali yaani kama ilivyokuwa kabla ya wanamgambo wa Hamas kuliteka eneo hilo la Gaza mnamo Juni iliyopita na kuvitimua vikosi vilivyokuwa tiifu kwa Rais Abbas.Lakini kundi la Hamas limepinga tangazo jipya la Fatah na kuongezea kuwa majadiliano yaliyopendekezwa kufanywa hayapewi umuhimu hivyo na chama cha Fatah.
Kwa upande mwingine,Makamu wa Rais wa Marekani Dick Cheney akifanya ziara yake ya kwanza katika Ukingo wa Magharibi tangu kushika wadhifa huo,alikutana na Rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas.Hapo awali alikuwa na majadiliano mbali mbali pamoja na viongozi wa Israel. Katika mkutano wa waandishi wa habari pamoja na Abbas,Cheney alilaani mashambulizi ya makombora yanayofanywa na wanamgambo wa Kipalestina dhidi ya Israel.Wakati huo huo Abbas alisema,katika jitahada za kutafuta amani Israel pia inapaswa kusitisha mashambulizi yake ya kijeshi na ujenzi wa makaazi mapya ya Wayahudi.Amesema itakuwa vigumu kupata usalama na amani wakati ujenzi wa maakazi ukiendelea na miji na vijiji vya Kipalestina vikizingirwa huku operesheni za kijeshi zikiendelea dhidi ya miji ya Wapalestina.
Makaazi ya Israel katika Ukingo wa Magharibi ni miongoni mwa vizuizi vikuu katika majadiliano ya amani tangu mazungumzo hayo kuanzishwa upya chini ya usimamizi wa Marekani Novemba mwaka jana.Cheney amesema,amani inaweza kupatikana iwapo pande zote zilizohusika zitashirikiana.Siku ya Jumamosi,Cheney alipokutana na Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert alisema makubaliano ya amani yatahitaji jitahada kubwa na kila upande utapaswa kuwa na maamuzi ya kuumiza.Ni matumaini ya Rais George W.Bush kuwa makubaliano ya amani yatapatikana,kabla ya kiongozi huyo kuondoka madarakani January mwaka 2009.Makamu wake Cheney amesema, wakati umewadia wa kuwa na taifa la Palestina na Wapalestina wanastahili hilo.