1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Farmajo ndiye rais mpya wa Somalia

8 Februari 2017

Waziri Mkuu wa zamani wa Somalia, Mohamed Abdullahi Farmajo, ameapishwa kuwa rais mpya wa nchi hiyo baada ya kushinda duru mbili za uchaguzi zilizofanywa na bunge Jumatano (08.02.2017) katika mji mkuu, Mogadishu.

https://p.dw.com/p/2XCCn
Somalia | Mohamed Abdullahi Farmajo
Picha: REUTERS/F. Omar

Miongoni mwa wagombea wote 21, hakuna aliyepata theluthi mbili ya kura zinazohitajika kushinda katika duru ya kwanza, na hivyo kulazimu kinyang'anyiro kikali kati ya wagombea wa kwanza, wa pili na wa tatu katika duru ya pili.

Farmajo, aliyeshindana na rais Hassan Sheikh Mohamud na rais wa zamani, Sharif Ahmed, alipata kura 184. Waziri mkuu huyo wa zamani angehitaji kura 219 kuepuka duru ya tatu, lakini Mohamud na Ahmed walikubali kushindwa baada ya kupata kura 97 na 46 mtawalia.

Farmajo, ambaye pia ana uraia wa Marekani, aliapa kupambana na rushwa na wanamgambo wa kundi la Al-Shabaab. Waziri mkuu huyo wa zamani ana umri wa miaka 55 na anatokea ukoo wa Darod. "Huu ndio mwanzo wa umoja wa taifa la Somalia, mwanzo wa vita dhidi ya Al-Shabaab na rushwa," alisema Farmajo baada ya kutangazwa mshindi kufuatia mchakato mrefu wa uchaguzi.

Shangwe na nderemo

Maelfu ya watu walijitokeza barabarani na wanajeshi walifyetua risasi angani kushangilia ushindi wa Farmajo, ambaye anaungwa mkono kwa kiasi kikubwa. "Ukurusa mpya umefunguliwa Somalia," alisema rais huyo mpya, na kumshukuru mtangulizi wake kwa kuliruhusu bunge kuepuka duru ya tatu ya uchaguzi.

Somalia Präsidentschaftswahl
Wabunge wa Somalia wakisubiri kupiga kura katika uchaguzi wa rais mjini MogadishuPicha: picture-alliance/AP Photo/F. Abdi

Kwa mujibu wa mwandishi wa shirika la habari la Ufaransa, AFP, wakimbizi wa kisomali katika kambi kubwa ya wakimbizi duniani ya Dadaab mashariki ya Kenya, pia walishangilia na kuimba wimbo wa taifa la Somalia waliposikia Farmajo alikuwa ameshinda uchaguzi wa rais. 

"Wakati umewadia kwa sisi Wasomali. Namshukuru Mungu. Huyu ndiye mtu tuliyemhitaji, anatujali, anawajali watu masikini, wanaume na wanawake," alisema Anfi Kassim, mzee wa umri wa miaka 60 ambaye amekuwa akiishi katika kambi ya Dadaab tangu mwaka 1992.

Ni uchaguzi muhimu

Waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa wanauona uchaguzi huo wa rais kuwa hatua muhimu kwa Somalia, taifa lililotumbukia katika machafuko baada ya kuanguka kwa utawala wa kiimla wa Mohamed Siad Barre mwaka 1991, na ambalo sasa linajizatiti kuimarisha demokrasia yake.

Somalia Präsidentschaftswahl
Spika wa bunge la Somalia, Mohamed Osman Jawari, kulia, akisubiri huku wabunge wakikusanyika kumchagua raisPicha: picture-alliance/abaca/S. Mohamed

Somalia, taifa linalopatikana katika pembe ya Afrika na linalokabiliwa na machafuko, liliamua kumchagua rais kupitia bunge kwa sababu masuala ya kiusalama na uhaba wa vifaa na nyenzo nyingine za uchaguzi, ulisababisha changamoto kubwa na kukwamisha juhudi za kuwezesha raia waliojiandikisha kama wapiga kura kutumia haki yao ya kupiga kura.

Afisa wa tume ya uchaguzi ya Somalia, ambaye hakutaka kutajwa jina, aliliambia shirika la habari la Ujerumani, dpa, kwamba uchaguzi wa rais ulihamishwa kutoka chuo cha mafunzo cha polisi hadi uwanja wa ndege katika mji mkuu, Mogadishu, kwa sababu za kiusalama.

Magari na safari za ndege zilipigwa marufuku na wanajeshi walipiga doria katika mji huo.

Mapema siku ya Jumatano wanamgambo wanaoshukiwa kuwa wanachama wa kundi la wanamgambo la Al-Shabaab, waliishambulia hoteli moja katika mji wa bandari wa Bosaso kaskazini mwa Somalia lakini wakakabiliwa na maafisa wa usalama. Maafisa wa eneo hilo walisema walinzi wanne na wanamgambo wawili waliuwawa katika makabiliano hayo.

Mwandishi:Josephat Charo/afp/dpa/reuters