1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Familia zakimbia mapigano kaskazini mwa Khartoum

7 Septemba 2024

Mamia ya familia zimeikimbia wilaya ya kaskazini mwa mji mkuu wa Sudan, Khartoum leo jumamosi kufuatia kuongezeka kwa mapigano kati ya jeshi la taifa na wanamgambo wa RSF karibu na kambi moja ya jeshi.

https://p.dw.com/p/4kOOU
Sudan| Mzozo wa kivita
Mamilioni ya watu wamekuwa wakimbizi tangu kuanza kwa mzozo nchini Sudan.Picha: UNCHCR

Mashuhuda wameliambia shirika la habari la AFP kwamba hali imekuwa tete kwenye wilaya ya Bahri na pande hasimu zinashambuliana vikali. Mkaazi mmoja amesema tangu mapema leo asubuhi jeshi limekuwa likivurumisha makombora kuelekea kusini mwa kambi ya jeshi ya Hattab huku ndege za kivita zikionekana kila wakati kwenye eneo hilo.

Shuhuda mwengine amesema wanamgambo wa RSF wamezishambulia nyumba za watu, wanawakamata raia na wengine wamewaua. Mapambano hayo yamezilazimisha familia nyingi kukimbia zikiwa zimebeba vitu vichache pekee vichwani.

Mapigano kati ya pande hizo hasimu yalizuka Aprili mwaka jana na tangu wakati huo yamesababisha vifo vya mamia kwa maelfu ya watu na mamilioni wengi wameyakimbia makaazi yao.