1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Familia za wapiganaji wa Taliban zawa ombaomba

29 Julai 2012

Familia nyingi za wapiganaji wa Kundi la Taliban waliouwawa katika mapigano dhidi ya Jeshi la Pakistan ama waliopoteza maisha yao nchini Afghanistan, sasa zinaishi katika umaskini mkubwa.

https://p.dw.com/p/15gGA
Wanawake wakiandamana kupinga kuuwawa kwa mwenzao na Taliban mjini Parwan, Afghanistan.

Taj Muhammad Khan, mwalimu wa Shule ya Tank, wilaya mojawapo kati ya 25 za mkoa wa Khyber Pakhtunkhwa karibu na kituo cha kijeshi cha Waziristan, maeneo yanayotawaliwa na Taliban anasema asilimia kubwa ya wajane na yatima wa wapiganaji hao sasa wanaombaomba mitaani, ili kujipatia chakula.

Khan ameliambia Shirika la Habari la IPS, kuwa hakuna mtu wa kuwasaidia familia hizo. Hata wakazi wa maeneo hao wanawadharau wajane na yatima hao, ambao watu waliokuwa wakiwategemea walijiunga na Kundi la Taliban na hatimaye kuuwawa na jeshi la serikali.

Taliban waliwahadaa watoto wetu

Mwalimu huyo anasema inasikitisha kuona, Wapiganaji wa Taliban waliwapa mafunzo ya kijeshi vijana hao wadogo na wasio na elimu, na sasa hawasaidii familia zao baada ya wapiganaji hao kupoteza maisha.

Muuza matunda mmoja mwenye umri wa miaka 28, Ikramullah Shah, aliondoka nyumbani kwake Tank mwezi Januari, akienda kuswali msikitini na tangu hapo hajarudi tena nyumbani, anaeleza baba wa kijana huyo, Abdullah Shah.

Shah anasema mwezi April, mwaka huu, baadhi ya viongozi wa Taliban walikuja nyumbani kwake usiku mmoja na kumtaarifu kuwa mwanae, yaani Ikramullah, amekuwa shahidi katika mapambano dhidi ya jeshi lililoasi. Kutokana na kifo hicho, Mzee huyo sasa anawajibika kulea mkamwanae wake na wajukuu, alioachiwa na muuza matunda huyo.

Rambirambi ya dola 400 haina thamani ya maisha ya mwanangu

Abdullah Shah anasema Taliban walimpatia dola 400, kufuatia msiba huo na wakamuahidi kuwa watakuwa wanampatia fedha kila mwezi za kujikimu kimaisha lakini ahadi hiyo imebaki kuwa maneno matupu, yasiyovunja mfupa.

Katika kisa kingine, mkulima mmoja kijana Shafqatullah kutoka Wilaya ya Charsadda aliuwawa nchini Afghanistan mwezi June, mwaka juzi. Shafqatullah aliyekuwa na umri wa miaka 21, alikuwa ndio tegemeo la wadogo zake wawili na wazazi wake. Sasa familia hiyo iko mashakani. .

Ni raia wa kawaida wanaopinga kundi la wapiganaji wa Taliban.
Ni raia wa kawaida wanaopinga kundi la wapiganaji wa Taliban.Picha: DW

Kiongozi mmoja wa ngazi ya juu, Syed Aqil, ameliambia Shirika la Habri la IPS, kuwa Taliban walikuwa ni mamluki ambao wamewatupa marafiki zao. Wameharibu maisha ya mamia ya familia kwa kuwahadaa vijana na kuwaingiza vitani na sasa hawapo tena, Taliban haijali familia zilizoachwa solemba.

Awali, kundi hilo linaloendesha shughuli zake Pakistan na Afghanistan lilikuwa likiwapatia misaada familio hizo, lakini sasa zinakabiliwa na ukosefu mkubwa wa fedha.

Taliban sasa taabani, baada ya ufadhili kusitishwa

Kufuatia juhudi za kimataifa za kuwasambaratisha wafadhili wa kikundi hicho cha kigaidi, Taliban sasa iko katika wakati mgumu kiuchumi. Msaada kwa familia hizo zilizopoteza wapendwa wao ulikatika tangu mwaka 2008.

Ofisa wa polisi, Muhammad Khalid, ambaye amechunguza kesi nyingi za aina hiyo, anasema familia huteseka kwa kiwango kikubwa sana wapiganaji hao wanapouwawa katika mapambano na jeshi. Anaongeza kusema kwamba mwanzoni Taliban ilitoa kifuta chozi kikubwa kwa baadhi ya warithi wa wapiganaji hao.

Katika miaka ya hivi karibuni, Taliban imewatelekeza wafuasi wao na familia zao katika Wilaya ya Mardan.

Mwandishi: Ndovie, Pendo Paul\ IPS

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman