Familia ya Bin Laden hii Saudia
27 Aprili 2012Kutoka nyumba waliyokuwa wakihifadhiwa kwa muda mjini Islamabad, Pakistan, waliingizwa kwenye gari dogo nyeupe yenye vioo vya giza na kupelekwa moja kwa moja uwanja wa ndege.
Mashahidi walimuona mwanamke mmoja akikataa kuingia ndani ya gari hiyo, akisukumwa kwa nguvu ndani ya gari, huku vyombo vya habari vikizunguka eneo hilo.
Ndege iliyotumwa na wizara ya mambo ya nje ya Saudi Arabia maalum kuichukua familia hiyo ya Bin Laden, iliruka saa 6 usiku na kufika nchini Saudi Arabia saa moja na nusu baadaye. Familia hiyo inajumuisha wajane watatu, watoto11 na wajukuu wanne wa kiongozi huyo ambaye aliweza kuitetemesha dunia kwa kipindi kirefu kabla ya kuuwawa na jeshi la Marekani Mei 2 mwaka jana.
Muhammad Amir Khalil ambaye ni mshauri wa mambo ya sheria kwa familia hiyo amesema mjane mdogo wa Osama bin Laden, Amal al Sadeh akiwa na kaka yake Zakariya al Sadeh na watoto wake watano watakuwepo Saudia kwa muda wakikamilisha masuala ya mirathi na mambo mengine ya kifamilia hiyo kabla ya kuelekea kwao Yemen.
Kabla ya kuanza safari ya kurudishwa Saudi Arabia, familia hiyo iliyokamatwa baada ya kuvamiwa na majeshi la Marekani na kuuwawa kwa Bin Laden, walishikiliwa kwa muda mrefu na vyombo vya usalama vya Marekani na Pakistan.
Mwisho walihukumiwa kifungo cha siku 45 kwa kuishi nchini Pakistan kinyume na sheria. Kwa kuwa walishakaa muda mrefu ndani, kifungo chao kilianza Aprili 2 na kumalizika Aprili 17 mwaka huu.
Kati ya wajane hao watatu wa Bin Laden, wawili ni raia wa Saudia Arabia na mwengine wa Yemen.
Hadi sasa haijafahamika ni vipi Bin Laden na familia yake waliweza kujificha katika jumba la Abbottabad umbali wa kilometa 61 Kaskazini Mashariki mwa Islamabad kabla ya kuvamiwa na majeshi ya Marekani.
Kikosi Maalum cha Jeshi la Kimarekani kiliivamia nyumba hiyo hapo Mei 2 mwaka jana, na kuripoti kwamba vilimuua Bin Laden wakati wa majibizano ya silaha. Hakuna uchunguzi zaidi uliotangazwa kuhusiana na tukio hilo hadi sasa.
Mwandishi:Adeladius Makwega/RTRE&DPAE
Mhariri: Mohammed Khelef