Falme ya nchi za Kiarabu ina magereza Yemen
23 Juni 2017Falme hiyo ni mwanachama mkuu wa ule muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia ulioingia Yemen mwaka 2015, kuiunga mkono serikali ya nchi hiyo inayopambana na waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran.
Maafisa wa Human Rights Watch walisema Ufalme wa nchi za Kiarabu unaonekana umewahamisha baadhi ya wafungwa wakuu nje ya nchi hiyo. Shirika hilo la kutetea haki za kibinadamu limeorodhesha visa 49 vikiwemo vya watoto wanne ambao walikuwa wamezuiliwa au kupotezwa kwa makusudi, 38 kati ya visa hivyo vikiwa vilifanywa na Milki za Kiarabu.
Shirika hilo lililo na makao yake New York, Marekani, lilisema pia Emirati ina jela kadhaa katika mikoa ya kusini ya Yemen ambayo ndiyo makao ya kundi la kigaidi la Al-Qaeda. Lilidai pia waasi wa Houthi na washirika wao, ambao ni wanajeshi waaminifu wa rais wa zamani Ali Abdullah Saleh, waliwazuia na kuwapoteza watu kadhaa kaskazini mwa Yemen.
Kipindupindu Yemen kimesababishwa na binadamu
Shirika la Afya Duniani WHO, linakadiria zaidi ya watu 8,000 wameuwawa katika kipindi cha miaka miwili ya mapigano nchini Yemen, ambayo inakabiliwa na mkurupuko wa maradhi ya kipindupindu na kitisho cha njaa.
Huku hayo yakiarifiwa mkuu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Stephen O'Brien, ameuelezea mripuko wa kipindipindu nchini Yemen, ambao kwa sasa unaelekea kufikia watu 300,000 walioathirika, kama janga lililosababishwa na binadamu.
"Hii ni kwasababu ya vita, ni jambo lililosababishwa na binadamu, ni baya sana, idadi ya watu walioathirika ni ya kushtua," alisema O'brien. "Suala la kipindupindu pamoja na ukosefu wa chakula, ukosefu wa huduma za matibabu bila shaka ni kutokana na hizo pande zote zilizo katika mapigano."
Wahusika wote wamechangia kusababisha janga la kibinadamu
Pande zote katika mzozo wa Yemen zimeshutumiwa kwa kusababisha raia wa nchi hiyo kuhangaika. Umoja wa Mataifa na Human Rights Watch walisema, mashambulizi ya angani yanayofanywa na muungano huo unaoongozwa na Saudi Arabia, yamewauwa raia wengi na huenda yakachukuliwa kama uhalifu wa kivita.
"Na sasa iwe ni wale wahusika wa moja kwa moja katika mapigano hayo au wanaowaunga mkono," alisema O'brien, "wote wanastahili kutambua kwamba wamechangia katika kusababisha janga la kibinadamu, ambapo ndiyo sehemu tuliyo nchini Yemen kwa sasa."
Uchambuzi wa shirika la habari la Reuters kuhusiana na hali ya kipindupindu Yemen kwa kutumia takwimu za shirika la Afya Duniani, unaonesha maambukizi yanaongezeka kwa asilimia 4 kila siku, huku idadi ya vifo vinavyotokana na maradhi hayo ikiongezeka kwa asilimia 3.5 kila siku.
Mwandishi: Jacob Safari/AFPE/Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu