1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Fainali za kombe la mataifa ya Ulaya-Euro 2008.

11 Juni 2008

Mashindano haya yanaendelea leo kwa msisimko mkubwa. Hapo jana Uhispania ilionyesha dimba la aina yake mbele ya Warusi huku Sweden ikawaadhibu mabingwa watetzezi Ugiriki.

https://p.dw.com/p/EHlv
Shabiki wa Ugiriki(mabingwa watetezi) akitafakari baada ya kulazwa na Sweden.Picha: AP

Tukianzia na Uhispania , pambano la jana dhidi ya Urusi lilikua dimba lililowainua mashabiki vitini, huku David Villa akiuona wavu mara tatu katika ushindi wao wa mabao 4-1. Warusi walionekana kuzidiwa ufundi ambapo safu ya ushambuliaji ya wahispania iliweza kuipangua ngome ya Urusi.

Uhispania kwa hivyo imejiunga na Ureno, Ujerumani na Uholanzi kuwa timu zilizoweza kuonyesha dimba la kuvutia zaidi, wakati mechi nane zimeshachezwa hadi sasa.

Katika mchuano mwengine Sweden ilifanikiwa kuwaangusha mabingwa watetezi wa kombe hilo Ugiriki mabao 2-0 yaliopachikwa katika kipindi cha pili. Ni Zlatan Ibrahimovic aliyekua wa kwanza kuuona wavu wa wagiriki, bao lake la kwanza akiwa na timu ya taifa katika muda wa miaka miwili.

Akizungumzia mchezo huo Kocha wa Ugiriki, Mjerumani Otto Rehhagel alisema,"Katika kipindi cha kwanza tuliweza kushambulia vyema kutoka nyuma na kubakia na matokeo ya bila kwa bila, lakini kosa la baadae sekunde moja tu likaipa Sweden bao la kwanza. Bila shaka Wasweden walicheza na kushambulia vizuri."

Leo hii wenyeji washirika na Austria ,Uswisi inamenyana na Uturuki ambapo kila moja itakua inawania ushindi kuweka matumaini ya kosonga mbele baada ya kupoteza mchezo wa awali na Ureno inapambana na Jamhuri ya Cheki.

Ama kwa Ujerumani itaingia uwanjani kesho dhidi ya Croatia ikikumbuka kipigo cha wakati wa mashindano ya kombe la dunia 1998 nchini Ufaransa ilipolazwa na Croatia katika robo fainali mabao 3-0.

Pamoja na hayo aliyekua kocha wa Croatia wakati huo Miroslav Blazevic anasema ana wasi wasi, kwani nikimnukuu anasema " wajerumani wakiwa uwanjani huwa kama mashine hata kama wanacheza bila ya mchezaji wa kuvutia. Anachoomba angalau ni sare kwani hiyo itaisaidia Croatia kupiga hatua kuelekea duru ya pili.

Sambamba na hayo inaonekana tayari mashabiki wa Croatia wameanza kushikwa na kihoro,Gazeti maarufu linalotoka kila siku 24 Sata lilikua na suali kwa kocha Slaven Bilic likimuuliza jee ameshaipata mbinu ya kuwaangusha wajerumani ? Na kusisitiza kwamba wakutupiwa macho zaidi ni washambuliaji wawili wa Ujerumani wenye asili ya Poland Miroslav Klose na Lukas Podolski.

Kivutio zaidi ya mashindano haya hadi sasa ni kwamba baada ya mechi nane hakuna kadi yoyote nyekundu iliyotolewa na muamuzi.