European Super League yatibuka
21 Aprili 2021Arsenal, Chelsea, Liverpool, Manchester United, Manchester City na Tottenham jana jioni walijiondoa katika mpango wa kuzindua mashindano hayo baada ya kuzuka kwa hasira miongoni mwa mashabiki wa soka huku serikali ya Uingereza pia ikionya kwamba hatua kali zingechukuliwa dhidi ya vilabu vitakavyoshiriki.
Wazo la kuanzishwa kwa European Super League lilitolewa na rais wa klabu ya Real Madrid Florentino Perez, ambaye pia alijumuisha timu za Uhispania Barcelona na Atletico Madrid pamoja na timu za Italia Juventus, AC Milan na Inter Milan.
Mmiliki mkuu wa Liverpool John Henry ameomba msamaha kwa mashabiki na kwa Kocha Juergen Klopp kwa usumbufu uliosababishwa na ushiriki wa klabu ya Liverpool katika uundaji wa European Super League.
"Nataka kuomba radhi kwa mashabiki wote wa Liverpool, kwa usumbufu niliousababisha katika muda wa saa 48 zilizopita. Lakini inapaswa kutambulika kuwa mpango wa michuano hio usingesimama bila mchango wa mashabiki.Hakuna mtu aliyewahi kufikiria tofauti nchini Uingereza. Katika saa 48 imekuwa wazi kabisa kwamba haitasimama. Tumewasikia. Nimesikia. Nataka kuomba msamaha kwa Jurgen (Klopp), kwa Billy Hogan, kwa wachezaji na kwa kila mtu ambaye alifanya kazi kwa bidii kwa Liverpool kuwafanya mashabiki wetu wajivunie. Hawahusiki kabisa katika usumbufu huu. Walikuwa wamevurugika zaidi na bila haki.Hii ndio inaumiza zaidi. Wanaipenda klabu na wanafanya kazi kuitengeneza ili mujivunie kila siku" amesema John Henry.
Muasisi wa European Super League ambaye pia ni mwenyekiti wa klabu ya Juventus Andrea Agnelli, alipoulizwa iwapo michuano hiyo itaendelea hata baada ya vilabu sita vya Uingereza kujiondoa.
"Tazama, nadhani niwe muwazi na mkweli : hapana, ni wazi kabisa haitakua hivyo kwa hivyo sitazungumza sana juu ya wapi mradi huo umekwenda, ninabaki na hakika juu ya uzuri wa mradi huo, na thamani ambayo ingepatikana ndani yake, ya kuunda mashindano bora ulimwenguni, lakini ni dhahiri hapana. Namaanisha, sidhani kuwa mradi huo bado utaendelea." amesema Andrea Agnelli.
Rais wa shrikisho la kandanda Ulaya, UEFA, Aleksander Ceferin amesema wanataka "kujenga tena umoja" ambao ni muhimu katika kuendelea kufurahia mchezo.
AP/Reuters/